Walichosema Dk Mabula, Gulamali baada ya CCM kuwatemwa

Dar es Salaam. Baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwatema waliokuwa wabunge wa Manonga, Seif Gulamali na Ilemela, Dk Angeline Mabula, wenyewe wameahidi kuendelea kukiunga mkono chama hicho na wagombea watakaoteuliwa.

Gulamali na Dk Angeline ni miongoni mwa wabunge zaidi ya 30 walioachwa katika orodha ya watiania ya ubunge wa majimbo na viti maalumu kwenda kwenye mchakato wa kupigiwa kura za maoni.

Hatua hiyo ilitangazwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alipozungumza na wanahabari jijini Dodoma jana Jumanne, Julai 28, 2025.

Wawili hao, kwa nyakati tofauti wamechapisha katika mitandao yao ya kijamii wakishukuru kwa utumishi wao wa miaka 10 bungeni, huku wakiahidi kuendelea kukiunga chama hicho.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Gulamali ameandika akijivunia utumishi wa miaka 10 bungeni akiwawakilisha wananchi wa Manonga, huku akiwatakia heri watiania waliopita kwenda hatua inayofuata.

“Tumeacha alama ambazo haziwezi kufutika katika maisha yetu yote. Tuendelee kukiunga mkono chama chetu, tumuunge mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kura za ushindi,” ameandika.

Katika chapisho lake hilo ameongeza; “Wote sisi ni washindi. Manonga ya maendeleo ndio ilikua kipaumbele chetu. Asanteni sana na Mwenyezi Mungu awabariki nyote.”

Historia ya Gulamali katika siasa, inaanzia Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), alikokuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Tabora.

Baada ya wadhifa huo, mwaka 2015 aliingia bungeni akiwawakilisha wananchi wa Manonga mkoani humo hadi mwaka 2025, kamati kuu ya chama hicho ilipomtema katika orodha ya watiania wa ubunge.

Kwa upande wa Dk Angeline naye amewatumikia wananchi wa Ilemela kwa miaka 10 tangu 2015. Kadhalika alilitumikia Taifa kwa nafasi ya Waziri wa Ardhi, Nyuma na Maendeleo ya Makazi, baada ya kuwa naibu kwa miaka kadhaa.

Katika ujumbe wake baada ya kuachwa kwenye orodha hiyo, Dk Angeline ametoa shukurani kwa utumishi huo wa miaka 10, huku akijivunia matokeo ya utendaji wake katika kipindi hicho.

Ameandika ni imani yake mwanachama yeyote wa chama hicho akiteuliwa ataendeleza pale alipoishia.

“Ninashukuru Mungu kwa heshima niliyopewa nyakati zote kutumikia chama na Serikali naheshimu uamuzi wa vikao kwa kuamua kila mwanachama wa CCM anayeomba kugombea ana sifa za kuchaguliwa,” amesema.

Ameahidi kushirikiana na chama chake kuhakikisha kinaendelea kushika dola, huku akiwapongeza wateule wote na kuwatakia kheri katika mchakato unaofuata.