Babati. Waliokuwa wabunge wa viti maalumu Mkoa wa Manyara, kwa kipindi kilichopita Regina Ndege na Yustina Rahhi wamefanikiwa kutetea nafasi zao kwa kuibuka kidedea kwenye kura za maoni.
Katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Babati leo jumatano Julai 30, 2025, Regina na Rahhi wamewashinda wagombea wenzao sita, kupitia kura 1,138 za wajumbe.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri akitangaza matokeo amesema Regina amepata kura 891.
Shekimweri amesema Rahhi amepata kura 703, Senorina. Wengine ni Jorojick (214), Joyclene Umbula (168), Loema Peter (90), Dk Pauline Nahato (71), Scolla Mollel (37) na Anna Shinini kura 23.
Akizungumza baada ya kutangazwa kushinda nafasi hiyo, Regina amewashukuru wajumbe kwa kumpa ridhaa ya kuendelea kuwawakilisha bungeni.
“Tulifanya kazi kubwa mwaka 2020/2025 na sasa mmenipa imani kubwa kwenu, nawaahidi kuendelea kuwatumika vyema kama awali na ninawashukuru mno kuendelea kuniamini,” amesema.
Kwa upande wake Rahhi amewashuku wajumbe hao kwa kumchagua kwani awali mwaka 2020/2025 alishika nafasi ya tatu na kuteuliwa baada ya Martha Umbula kufariki dunia.
“Nawashukuru kwa kunipa heshima kubwa tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha kuwa jamii inaendelea kupiga hatua kwenye masuala mbalimbali,” amesema Rahhi.