Musoma. Wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Mara, wameahidi kuchagua wawakilishi wenye uwezo wa kuwawakilisha vema sambamba na kuwaunganisha.
Jumla ya wajumbe 1,435 wanashiriki mkutano huo leo Jumatano Julai 30, 2025 kwa lengo la kuchagua majina ya wabunge wawili kati ya wagombea wanane ambao majina yao yamerudishwa na vikao vya CCM kwa ajili ya kupigwa kura za maoni.
Upigaji kura hizo za maoni, unalenga kuwapata wagombea ubunge wa viti maalumu kutoka Mkoa wa Mara kupitia CCM.
“Tunataka maendeleo, tunataka mbunge anayejua wajibu wake, tunataka mbunge atakayetuunganisha wanawake na sio kutugawa, kwa ufupi tunawataka wabunge wanaojitambua,” amesema Asha Swalehe alipozungumza na Mwananchi.
Asha ambaye ni mjumbe wa UWT, amesema watatimiza wajibu wao kwa kuwapigia kura za maoni wabunge wanaofaa hasa kwa kuangalia sifa na vigezo vya uongozi na si umaarufu wao.
Naye Nyageti Adam amesema wabunge watakaochaguliwa wanapaswa kutambua kuwa wanalo jukumu kubwa la kuwawakilisha wananchi hasa wanawake wa Mkoa wa Mara katika Bunge la Tanzania, ambalo wanatakiwa kulifanya kwa ufanisi mkubwa.
“Hatutaki viongozi ambao wakishachaguliwa wanatimkia huko na kutuacha, tunataka wawakilishi wa wanawake wa Mkoa wa Mara watakaozisemea changamoto za wanawake ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na si vinginevyo,” amesema Nyageti.
Mwananchi pia imezungumza na Naima Minga ambaye amesema UWT Mkoa wa Mara wamejipanga kuwachagua wabunge watakaokuwa daraja kati ya wanawake wa mkoa huo na Serikali kupitia Bunge.
Amesema wanawake wanahitaji uwezeshaji kiuchumi kusudi waondokane na changamoto mbalimbali, “hivyo wajumbe kwa kulitambua hili kwa pamoja tutawachagua wawakilishi wenye sifa.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mara, Ndeni Amos amesema maandalizi yote yamekamilika na uchaguzi huo unatarajiwa kuwa huru na haki na, kila mgombea atatendewa haki.
Tayari wagombea wote wanane wameingia ukumbini na ili kudhibiti vitendo vya rushwa pamoja na mambo mengine, limetolewa tangazo linalowataka kila mmoja kutokuwa na fedha taslimu zaidi ya Sh50,000 kwenye pochi au mifuko yake.
Kutokana na tangazo hilo, baadhi ya wagombea waliokuwa na fedha zaidi ya kiasi hicho wameonekana wakizikabidhi kwa ndugu na jamaa.