Watia nia UWT Dar waanza kujinadi, ukumbi wafurika wajumbe

Dar es Salaam. Mchakato wa watia nia kujinadi mbele ya wajumbe kwa ajili ya kuwashawishi wawachague kuwa wabunge wa viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), umeanza rasmi katika Ukumbi wa Karume Hall, Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imefuatia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyefungua mkutano huo kwa kuwasihi wajumbe kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia masilahi mapana ya wanawake wote nchini, sambamba na ustawi wa chama hicho alichosema kinaaminiwa na Watanzania wengi.

Uchaguzi huo unafanyika leo Jumatano Julai 30, 2025 baada ya Kamati Kuu ya CCM kufanya mchujo na kuteua majina tisa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ambayo yalitangazwa jana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla.

Baadhi ya wajumbe wa UWT mkoa wa Dar es Salaam,  wakiwa nje ya Ukumbi baada ya kumaliza shughuli ya upigaji kura, sasa wanasubiri matokeo.

Makada waliofanikiwa kuingia hatua hiyo ya mwisho na wanaowania nafasi hiyo ni Janeth Mahawanga, Neema Kiusa (Mwenyekiti wa UWT, Ilala), Doreen Kahwa, Mossy Msindo, Maida Juma, Amina Said, Georgina Lukwembe, Janejelly Ntante na Zainab Jangu.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave, nafasi zinazowaniwa ni mbili, ingawa kuna uwezekano wa kuongezeka hadi tatu endapo kutatokea ongezeko la kura baada ya kupatikana kwa wabunge wa majimbo.

Kazi ya upigaji kura inaendelea kwa utulivu, huku baadhi ya wajumbe wakianza kutoka nje ya ukumbi baada ya kukamilisha wajibu wao. Jumla ya wajumbe 842 walitarajiwa kushiriki, lakini waliojitokeza kupiga kura ni 811.

Baadhi ya wajumbe wamepongeza utaratibu wa mchakato huo kwa kueleza kuwa ni mzuri na hauna mlolongo mrefu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Nimeshapiga kura, sasa nasubiri matokeo rasmi kujua ni nani kati ya hawa wagombea atakuwa amepata ridhaa ya kuwa mwakilishi wa wanawake wa Mkoa wetu wa Dar es Salaam kupitia UWT,” amesema mjumbe mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake.