Dar es Salaam. Ili kuhakikisha kila mmoja anafikiwa na fursa za kukua kiuchumi bila kujali hali yake, watu takriban 5,000 wenye uhitaji maalumu nchini wameanza kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi.
Ufundi huo unajumuisha kuchomelea, ushoni, kuandaa mapishi katika vyuo vya Mamlaka ya Elimu Mafunzo ya Ufundi (Veta), Chang’ombe, Yombo na jijini Mbeya.
Akizungumza Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo Veta, Angelus Ngonyani amesema zaidi ya vijana 5,000 wenye ulemavu watanufaika na mradi huo wa mafunzo jumuishi ya ufundi stadi ili waweze kujiajiri kupitia ujuzi huo.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kufunga mradi huo uliofadhiliwa na shirika la maendeleo la CEFA, huku mwakilishi mkaazi wa CEFA Tanzania, Cinzia D’intino akisema mradi umejumuisha utoaji wa vifaa kwenye vyuo vitatu vya Veta Tanzania, utoaji wa mafunzo kwa walimu ili kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Pia, mradi unawaongezea walimu mbinu za mafunzo kwa watu wenye uhitaji maalumu. Hadi sasa vimefikiwa vyuo vya Veta Chang’ombe, yombo na jijini Mbeya,” amesema Ngonyani.
Amesema mradi huo umetoa mwongozo wa ufundishaji kwa walimu kwa watu wenye ulemavu kwasababu ni jambo la msingi na walimu wetu hawakuwa na uwezo mkubwa wa kuwafundisha watu wenye mahitaji maalumu.
“Tumepata pia vifaa vya kufundishia na kujifunzia vifaa vya kisasa na huu umetupa mwanga katika kuwafundisha watu hawa wenye mahitaji,” amesema.
Akieleza zaidi kuhusu mradi huo, D’intino amesema umejumuisha utoaji wa vifaa kwenye vyuo vitatu vya Veta Tanzania na utoaji wa mafunzo kwa walimu ili kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Tumeendelea kuunga mkono uwezeshaji wa watu wenye mahitaji maalumu kupitia elimu pia katika kuhakikisha ujumuishaji wa makundi yote ya jamii,” amesema D’intino.
Mshauri wa masuala ya ujumuishwaji kwa watu wenye ulemavu, Francis Gugu amesema walimu wa vyuo vya Veta wamepata uwezo wa kuwafundisha wanafunzi hao wenye hali tofauti za ulemavu wakiwemo wenye changamoto ya usonji.

“Wanafunzi wenye ulemavu sasa wanapata fursa ya kujifunza kwa namna ya urafiki zaidi na zile changamoto za kimazingira zimeondoka,” ameeleza.
Mnufaika wa mradi huo, Rehema Abdallah amesema mradi umekuwa fursa kwake kwa kuwa amekuwa akiishi nyumbami muda wote bila shughuli ya kufanya.
“Kwasasahivi ninao uwezo wa kwenda mahali popote kuomba kazi na nikapata kwasababu nimejifunza uandaaji wa chakula,” amesema Rehema.