Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema ipo katika hatua za mwisho kukamilisha sera ya maafa itakayotoa mwongozo wa namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali, kuzuia au kupunguza vifo vinavyotokana na tatizo hilo ikiwemo watu kuzama majini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Islam Seif Salim leo Julai 30, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzama majini.
Kila ifikapo Julai 25 hadi 28 dunia huadhimisha siku ya kuzama majini, ambapo kwa Zanzibar imeadhimishwa leo.
Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na kutoa mafunzo na kuwashindanisha wanafunzi wa shule mbalimbali kuhusu namna ya kuogelea ili kujilinda na maafa pindi yanapotokea.
“Serikali inahakikisha inaweka mipango ya kuokoa, kulinda na kupunguza matatizo ya vifo vinavyotokana na maafa na katika kuhakikisha hilo, Serikali ipo katika hatua za mwisho kuandaa sera ya maafa ya mwaka 2025 ambayo itatoa mwanga na kuweka misingi ya kuzuia yasitokee,” amesema Dk Seif.
Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh amesema taasisi zote zinazohusika na maafa ni vema zikajikita kulinda yasitokee badala ya kusubiri yatokee kisha waje kuokoa.
Amesema kuna vifo ambavyo vinazuilika vya watu kuzama baharini kwani baadhi hawajui kuogelea na hakuna kasumba ya kuokoana, kwa hiyo inatakiwa kuchukuliwa jitihada za makusudi kusaidia hali hiyo.
“Tuwafundishe watoto huko shuleni, wajue kuogelea na namna ya kuokoana, hakika kuna vifo ambavyo vinaepukika na taasisi zinazohusika na maafa ziwe na mikakati ya kukinga maafa yasitokee ambayo yanawezekana kukingwa, badala ya kusubiri yatokee twende kukimbiza kuokoa,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame amesema kuzama kunasababisha vifo na ulemavu, lakini kwa sasa inatoa elimu kwa wakulima wa mwani ikiwa ni sehemu ya mpango kazi wa mwaka 2024/25.
Ametaja miongoni mwa changamoto zinazokabili masuala ya uokozi kuwa ni pamoja na kutokuwa na doria katika maeneo ya mabwawa wanapokuwa wanaogelea wananchi, huku kukitakiwa kuwa na walinzi katika maeneo yote ya fukwe za hoteli.
“Tunapaswa kuongeza kwenye mitalaa shuleni kuhusu masuala ya maafa na uokozi, na kuwa na kanuni zinazolazimisha kuwapo kwa vifaa vya uokozi kwani jambo hilo ni mtambuka kila mmoja anaguswa nalo kwa namna moja ama nyingine,” amesema.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Ali Omar Ali amesema kuzama kunaweza kuzuilika iwapo kukiwa na elimu na watu kuzingatia misingi yake.
“Mazingira yetu ni ya kisiwa, yamezungukwa na maji, lakini iwapo wananchi wakielewa na kuzingatia misingi basi itazuilika maana kuzama sio tu baharini hata kwenye beseni, mabwawa na mito watoto wanazama na kupoteza maisha,” amesema.
Naye mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) Ofisi ya Zanzibar, Marco Msambazi amesema watoto ni rahisi kuathirika na hali hiyo, hivyo ni vyema wakifundishwa namna ya kuepuka kuzama.