Bandari Kwala itakavyopunguza msongamano barabarani Dar

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge amesema kuanza kazi kwa treni ya kupeleka mizigo katika Bandari kavu ya Kwala kutoka bandari ya Dar es Salaam kutasaidia kupunguza msongamano wa magari kwa asilimia 30.

Ametoa kauli hiyo wakati akitoa salamu za mkoa wake katika hafla ya ufunguzi wa Bandari kavu ya Kwala yenye ukubwa wa hekta 502 ikiwa ni mara tano ya bandari yote ya Dar es Salaam,  na mpaka sasa eneo lililozungushiwa ukuta ni hekta 60.

Bandari hiyo kavu umezinduliwa leo Alhamisi Julai 31, 2025 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Kunenge amesema barabara Tanzam inapitisha magari 1,600 kwa siku ambapo asilimia 60 ya magari hayo ni makubwa hivyo kwa kuanza reli hiyo itapunguza msongamano kwa asilimia 30.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri wa treni ya umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma eneo la Kwala Marshalling Yard mkoani Pwani, leo Julai 31, 2025.



“Si hilo tu, nikushukuru kwa niaba ya wakazi wa Pwani kwa uamuzi wa kuweka kituo cha treni hapa Kwala na kuweka, treni itakayokuwa ikisafirisha watu kutoka Pwani kwenda Dar es Salaam,” amesema.

Hilo litashuhudiwa kutokana na magari kutokuwa na ulazima wa kufika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kubeba mizigo na badala yake magari hayo yataishia katika bandari ya Kwala.

Mbali na hilo, Kunenge amelivunia mkoa wake kuwa na idadi kubwa ya viwanda ambapo vimefikia 1,681.

Amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani Machi 19, 2021 viwanda vikubwa vilikuwa 59 na sasa viko 97, viwanda vya kati vilikuwa 109 sasa vimeongezeka 71.

Amesema kwa sasa viwanda 26 katika vile vikubwa viko hatua mbalimbali za kukamilika na vingine tisa vya kati vikiwa hatua mbalimbali.

“Viwanda hivyo vimetoa ajira za moja kwa moja 21,000 na zisizo za moja kwa moja 60,000. Sasa hivi ukienda hospitali ukakuta mwananchi anawekewa dripu ya Tanzania na zinatoka Pwani hatuagizi tena. Sasa hivi televisheni tunatengeneza Pwani, Simujanja zinazalishwa Pwani na tayari ziko sokoni,” amesema Kunenge.

Amesema pia wanavyo viwanda vitatu vya kubangua korosho huku akiweka bayana kuwa mkoa huo unazalisha nondo, dawa za binadamu na wanaunganisha magari kupitia viwanda vitatu walivyonavyo.

Amesema wakati Samia anaingia madarakani walikuwa na changamoto ya umeme na kwa siku walikuwa wakipata megawati 70 ikaongezeka hadi 118 na sasa wanapata megawati 140, huku mwakani wakitarajia kupata megawati 168.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya kuwezesha Usafirishaji wa Ushoroba wa Kati (Central Corridor), Flory Okandju amesema Tanzania inaendelea kujijenga kama lango muhimu na lenye gharama nafuu kwa masoko ya kikanda.


Amesema Wakala wa Ushoroba wa Kati ni taasisi ya serikali za nchi mbalimbali yenye makao yake makuu Tanzania, ambayo imepewa jukumu la kuwezesha usafiri wa kupitisha mizigo na biashara kutoka na kwenda bandari za Tanzania kwa nchi zisizo na bandari kwa kutumia njia mbalimbali za usafiri.

“Kwa muktadha huu, tulichukua hatua muhimu ya kuliunga mkono Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kufadhili ukarabati wa mabehewa ya mizigo 20 kwa kutumia Sh1 bilioni ili kuongeza upatikanaji wa mabehewa na uwezo wa kubeba mizigo katika Ushoroba ya Kati,” amesema.

Amesema mabehewa hayo yana uwezo wa kubeba tani 800 kwa mara moja na hivyo kupunguza msongamano kwenye mtandao wa barabara za kikanda.

Amesema pamoja na mabehewa hayo yaliyokarabatiwa, Ushoroba wa Kati inaendeleza diplomasia ya kiuchumi na baadhi ya juhudi zinazofanyika kwa sasa ni pamoja na kuisaidia Burundi, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda kuanzisha bandari kavu za kisasa Kwala na Isaka.

Kwa sasa ujenzi wa kituo cha Burundi katika eneo la Kwala unaendelea na mazungumzo na wawekezaji binafsi kwa ajili ya Rwanda-Isaka na DRC-Kwala yanaendelea.

“Tunaendelea kuratibu juhudi za pamoja za maendeleo ya reli kati ya Tanzania na Burundi (SDRA) sehemu ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni na kuwezesha upembuzi yakinifu wa sehemu ya Burundi–DRC, ambao inatarajiwa kukamilika mwaka ujao,” amesema.

Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika jitihada za Tanzania kuboresha miundombinu ya usafirishaji, kupunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam na kuboresha usafirishaji wa mizigo kuelekea bara na nchi jirani.

Amesema WFP imekuwa sehemu muhimu ya kazi ya muda mrefu ya Serikali ya Tanzania katika kuwezesha usafirishaji wa bidhaa za misaada ya chakula ya kibinadamu, ikiwamo ya  kutoka nje au zinazozalishwa nchini kuelekea nchi jirani katika ukanda huo, zikiwemo DRC, Burundi, Rwanda, Uganda, Sudan Kusini, Kenya, Malawi, na Zambia.

Kufuatia hilo, Machi 2019 kupitia makubaliano ya ushirikiano (MOU) yaliyosainiwa na DRC, WFP iliwekeza dola 500,000 za Marekani (Sh1.27 bilioni) kwa ajili ya kukarabati mabehewa 40 ya mizigo.

“Juhudi hii ililenga kuongeza uwezo wa kiutendaji wa DRC, kwa kutoa kipaumbele katika kusafirisha bidhaa za chakula za misaada ya kibinadamu kupitia Ushoroba wa Kati. Katika miaka ya 2024 na 2025 pia WFP ilisafirisha zaidi ya tani 10,000 za chakula kupitia reli ya kati,” amesema.

Amesema mabadiliko hayo ya njia ya usafirishaji yamesababisha kupungua kwa gharama kwa takriban asilimia 37 na kupungua kwa utoaji wa hewa ya ukaa ikilinganishwa na usafiri wa barabara, na kuchangia dola 600,000 za Marekani (Sh1.53 bilioni) kwa sekta ya reli.