BOOST YALETA MAGEUZI YA TEHAMA WALIMU WAJIVUNIA UJUZI MPYA

Mradi wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) imewezesha vifaa vya TEHAMA katika shule teule na vituo vya walimu 400 ili kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji kwa njia za kisasa.

Aidha imewajengea uwezo walimu 600 wa TEHAMA, walimu wakuu 600, na waratibu elimu kata 450 namna ya kutumia vifaa hivyo kwa tija katika mazingira ya kufundishia.

Mwalimu wa TEHAMA katika Shule ya Msingi Ramadhani iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe Silivia Mbilinyi, amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko katika mbinu za kufundishia, na sasa wanafunzi wanashiriki kikamilifu darasani kupitia matumizi ya vifaa vya TEHAMA.

Naye, mwalimu Erasto William katika Shule ya Msingi Nyambogo iliyopo katika Halmashauri ya Makambako amesema kuwa walimu wengi wameweza kubuni mbinu bunifu za kufundisha, na hivyo kuifanya elimu kuwa ya kuvutia na ya kisasa zaidi kwa wanafunzi wa shule za msingi.