Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini kimemsimamisha Katibu wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, Odero Odero kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Odero ambaye alikuwa miongoni mwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti ndani ya Chadema, majukumu yake kama mjumbe sekretarieti ya kanda pia yatasimama.
Katika uchaguzi wa ndani wa Chadema uliofanyika Januari 21, 2025 alikuwa akichuana na Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi ya uenyekiti na Tundu Lissu ambaye mwisho wa uchaguzi aliibuka mshindi.
Odero alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura moja. Lissu alipata kura 513 na Mbowe akipata kura 482. Jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 999 na halali zikiwa 996 huku tatu zikiharibika.
Taarifa ya kusimamishwa kwa Odero ndani ya Chadema Kanda ya Kaskazini imetolewa jana Jumatano, Julai 30, 2025 na Katibu Kanda ya Kaskazini, Ndonde Totinan baada ya kupokea tuhuma dhidi ya kada huyo kuwa mwenendo usioridhisha.
“Kutokana na uzito wa tuhuma zilizotolewa dhidi yake na katika kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote mbili, Odero Odero kwa sasa atasimama kuwa Katibu wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu ili kuipa nafasi ofisi yangu kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma dhidi yako,” imeeleza.
“Ikizingatiwa pia, Odero ni mjumbe sekretarieti ya kanda yenye mikoa minne ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Hivyo, ili kuondoa mgongano wa kimaslahi atapisha uchunguzi huru dhidi yake,” imeelezwa kwenye taarifa hiyo.
Toitan amesema suala hilo litawasilishwa katika kamati ya maadili ya kanda na kupewa fursa ya kujulishwa tuhuma dhidi yake na haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama ili kuhakikisha haki inatendeka.
“Baada ya hatua zote kukamilika tutatoa taarifa kuhusu uamuzi utakaofikiwa. Naomba tuwe watulivu na kuendelea na mapambano ya No reforms, no election,” amesema Toitan.
Asubuhi ya leo Alhamisi, Julai 30, 2025, Mwananchi limemtafuta Odero ambaye amesema barua ya kusimamishwa kwake aliipokea usiku wa jana Jumatano. Hata hivyo, hakueleza kwa kina tuhuma hizo zinazoelezwa iwapo anazifahamu.