Devotha na Samira waibuka washindi Uchaguzi wa UWT Kagera

 Na Diana Byera, Bukoba

Devotha Daniel Mburarugaba na Samira Khalfani Amour wameibuka washindi kati ya wagombea nane walioshiriki katika uchaguzi wa kura za maoni nafasi ya ubunge wa viti maalum mkoa wa Kagera kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu UWT Taifa, Yasmin Bachu, alisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa na wagombea nane na jumla ya wapiga kura walikuwa 1,483 ambapo kura moja iliharibika, hivyo kura halali zilikuwa 1,482.

Bachu aliwataja Devotha Daniel aliyepata kura 1,308 na Samira Khalfani 1,250 kuwa ndio walioongoza katika uchaguzi huo, wakifuatiwa na Anitha Korongo aliyepata kura 153, Elizabeth Ngaiza kura 94, Anitha Bunono kura 52, Anitha Nyamzinga kura 44, Herieth Lugaju kura 37 na Evastina Godian kura 26.

Aidha, Bachu amewashauri wajumbe wa UWT mkoa wa Kagera kuwa wakati wa kampeni za Dk. Samia Suluhu Hassan wapaze sauti na kuunganisha nguvu kumuombea kura za kutosha, pamoja na kushinda majimbo yote ya mkoa wa Kagera ili kuwawezesha washindi hao wawili kuingia bungeni.

Wagombea hao wamesema kuwa uchaguzi uliendeshwa katika mazingira safi na salama ya hali ya juu, na kuwaomba wenzao ambao kura hazikutosha waendelee kushirikiana na waliochaguliwa kufanya kazi pamoja kwa kuwa wote ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.

Devotha Daniel aliwaomba wajumbe kuungana na kuondoa makundi kwa kuwa uchaguzi umeshapita na sasa wawe kitu kimoja. Amesema wote walikuwa wazuri, na sasa wanajenga nyumba moja hivyo ni muhimu kushirikiana ili kutafuta kura za Dk. Samia na majimbo yote nane kwa urahisi, kwani ndilo jambo kubwa lililopo mbele yao kwa sasa.

Kwa upande wake, Samira Khalfani alishukuru Kamati ya CCM Taifa kwa kurudisha jina lake na kumuona anafaa katika nafasi hiyo. Pia aliwaasa wagombea wenzake ambao hawakufanikiwa kupata ushindi wasikate tamaa kwani ndani ya chama hicho kuna nafasi nyingi, hivyo zinapotokea wasisite kugombea kwa kuwa wote wanahitaji kutafuta kura usiku na mchana ili CCM ishinde.

Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kagera, Hajat Faidhah Kainamula, alisema kuwa katika zoezi la kupata mgombea, lipo suala la kupatikana na kukosa kuchaguliwa. Jambo la muhimu kwa sasa ni wajumbe kushikamana ili kuleta maendeleo mazuri ndani ya chama na siyo marumbano.

“Tuondoe chuki, baada ya uchaguzi kinachotakiwa katika chama ni mshikamano wenye kutenda, utekelezaji na kupata mafanikio mazuri yatakayoleta maendeleo,” alisema Kainamula.

Katibu wa UWT mkoa wa Kagera, Rehema Zuberi, alisema kuwa awali watia nia wa nafasi za viti maalum walikuwa 13, ambapo mmoja hakurudisha fomu. Wagombea wanane waliteuliwa na Kamati Kuu kugombea huku wagombea wanne hawakuteuliwa.