Ecua, Boyeli mtegoni Yanga, Mzize, Dube waletewa mtaalamu mpya

KUNA kazi kubwa ipo pale Yanga ambayo inawahusu nyota wa kikosi hicho wanaocheza nafasi ya ushambuliaji lakini pia ikiwagusa wapinzani wao, huku maingizo mapya Celestin Ecua na Andy Boyeli yakiwa mtegoni.

Yanga iliyomaliza msimu wa 2024-2025 ikitwaa mataji matano yakiwamo manne ya ndani ambayo ni Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, ina kibarua kizito cha kuyatetetea msimu ujao 2025-2026.

Katika kibarua hicho, imeendelea kuimarisha kikosi chake huku eneo ambalo limekuwa na maboresho makubwa ni safu ya ushambuliaji ripoti zikibainisha timu hiyo imewasajili washambuliaji Celestin Ecua kutoka Zoman FC ya Ivory Coast ambapo msimu uliopita alicheza Asec Mimosas akiibuka Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu nchini humo akihusika na mabao 27 katika mechi 30 akifunga mabao 15 na kuasisti 12.

Mwingine ni Andy Boyeli raia wa DR Congo aliyetokea Sekhukhune United ya Afrika Kusini akiwa chaguo la kocha Romain Folz wakati anatua.

Nyota hao wapya wa eneo la ushambuliaji wanakuja kuungana na Clement Mzize na Prince Dube ambao msimu uliopita waliiongoza safu hiyo vizuri wakifunga jumla ya mabao 27. Mzize akifunga 14 na Dube 13.

Safu hiyo ya ushambuliaji inayoundwa pia na viungo, ilikuwa na mchango mkubwa wa kufunga mabao msimu uliopita kwenye michuano yote iliyoshiriki ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Kwa jumla, kwenye michuano hiyo mitano iliyoshiriki Yanga msimu uliopita, ilifunga jumla ya mabao 136 ikiwa ndiyo timu iliyokuwa na mabao mengi zaidi. Mchanganuo wa mabao hayo upo hivi; Ngao ya Jamii (5), Ligi Kuu Bara (83), Ligi ya Mabingwa Afrika (22), Kombe la FA (22) na Kombe la Muungano (4), hivyo msimu ujao kuna kazi kubwa ya kufikia idadi hiyo ya mabao mbali na kubeba mataji.

Ukiachana na nyota hao kuwa tishio kwa wapinzani, pia ndani ya kikosi cha Yanga kutakuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kuwania nafasi ya kuanza kucheza.

Tulishuhudia msimu uliopita, benchi la ufundi la Yanga chini ya Miguel Gamondi ambaye alianza msimu, kabla ya kuondolewa Novemba 2024 alikuwa akimtumia zaidi Dube kama mshambuliaji wa mwisho, huku Mzize wakati mwingine akitokea benchini, huku mara chache zaidi akiwatumia pamoja.

Mwendelezo huo ukawa pia kwa Sead Ramovic, lakini alipotua Miloud Hamdi, mara nyingi akawa anawatumia wote kwa pamoja na kuzifanya safu za ulinzi za wapinzani kuwa na wakati mgumu sana.

Wakati Dube na Mzize wakicheza, Kennedy Musonda ambaye naye alikuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, alikuwa akikaa sana benchini na mkataba wake ulipomalizika mwisho wa msimu akaondoka na sasa ametambulishwa Hapoel Ramat Gan Givatayim ya Israel.

Dube ambaye kiasili ni mshambuliaji wa mwisho, ana kazi ya kuwania nafasi ya kuanza mbele ya Boyeli, huku Mzize anayetokea pembeni, mshindani wake akiwa Ecua.

Ukiangalia vita ya nyota hao, muamuzi wa mwisho ni benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha mkuu, Romain Folz ambaye naye ana jukumu la kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo iliyojiwekea ikiwamo kutetea mataji iliyoshinda msimu uliopita na kucheza tena hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika kufikia malengo hayo, lazima ajenge kikosi imara kitakachokuwa kikimpa matokeo chanya kila kinaposhuka dimbani, lakini kubwa zaidi, nyota hao kuingia kwenye falsafa zake.

Folz ni mmoja wa makocha Afrika wanaopendelea mfumo wa 4-3-3, huku akisisitiza nidhamu ya ulinzi kabla ya kushambulia tofauti kabisa na mifumo ya kushambulia isiyojali usalama wa safu ya nyuma.

Katika mfumo wa Folz, viungo wa pembeni hawatakiwi kupoteza nafasi kiholela, mabeki wa pembeni wanapewa majukumu ya msingi ya kujilinda kabla ya kushambulia, na kiungo mkabaji hubeba jukumu la kiungo wa mpito ambaye huamua kasi ya mchezo.

Ni mfumo unaojenga timu ngumu kufungika lakini pia unahitaji wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu. Kwenye mazingira ya Yanga ambayo imezoea kushambulia kwa nguvu kupitia mawinga kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na washambuliaji kama Prince Dube, mfumo huu unaweza kuibua changamoto ya kimbinu iwapo wachezaji hawatamudu mabadiliko hayo.

Ujio wa Ecua ambaye pia ana uwezo wa kucheza kutokea pembeni, unaweza kumpa wakati mzuri kocha Folz katika mbinu zake ndani ya uwanja kutokana na nyota huyo kufanya mambo makubwa alikotoka.

Haya yote yakiwa yanaendelea, Yanga imeunda benchi jipya la ufundi lenye watu sita wapya ambao ni Romain Folz (kocha mkuu), Manu Rodriguez (kocha msaidizi), Majdi Ben Mansour Mnasria (kocha wa makipa), Thulani Thekiso (mchambuzi wa video), Chyna Tshephang Mokaila (kocha wa viungo) na Paul Matthews (mkurugenzi wa ufundi).

Katika watu hao sita, kuna mmoja ambaye ni mtaalamu zaidi wa kuwanoa washambuliaji, hali inayofanya msimu ujao Yanga huenda ikawa na makali zaidi eneo hilo.

Mtaalamu huyo ni Manu Rodriguez, licha ya kwamba anatambulika kama kocha msaidizi, pia amebobea katika kuwanoa washambuliaji akifanya kazi hiyo katika klabu kubwa Ulaya ikiwamo Real Madrid ya Hispania na Olympique Lyon ya Ufaransa. Pia mtaalamu wa kukuza vipaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA).

Uwepo wa mtaalamu huyo ndani ya Yanga ni kitu kipya ingawa imeshawahi kufanywa na Azam FC ilipomuajiri Kally Ongala kuwa kocha wa washambuliaji kikosini hapo msimu wa 2022-2023.

Pia Klabu ya Manchester United inayoshiriki Ligi Kuu England iliwahi kumuajiri straika wa zamani wa Afrika Kusini, Benni McCarthy kuwa kocha wa washambuliaji kikosini hapo kwa misimu miwili 2022-2023 na 2023-2024 chini ya kocha mkuu, Erik ten Hag.