Hongera Mfaume huo ndiyo uanamichezo sasa

JUMAMOSI ya wiki iliyopita mapambano ya ngumi yaliyopigwa pale katika Viwanja vya Leaders Kinondoni yaliacha mijadala mikubwa baada ya kumalizika kwake.

Mapambano mawili ndio yalijadiliwa sana ambayo moja ni la Mfaume Mfaume dhidi ya Kudakwache Banda kutoka Malawi na lingine lilikuwa la Ibrahim Classic dhidi ya Ramadhan Nassibu.

Mfaume aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya Banda na majaji wakaamua pambano baina ya Nassibu na Classic ni sare lakini kundi kubwa tuliotazama mapambano hayo hatukuridhishwa.

Sisi hapa kijiweni wengi tuliamini yule Mmalawi alistahili kuibuka mshindi dhidi ya ndugu yetu Mfaume maana alicheza vizuri sana ila mwishowe majaji wakaamua kumpa wa nyumbani.

Hata lile pambano la Classic na Nassibu, wengi tulihisi ushindi ungeenda kwa Rama lakini majaji wakatusapraizi kwa kuitoa ngoma pacha ila ndio tutafanyaje sasa na wao ndiyo waamuzi wa mwisho sisi tutabaki kushangaa tu.

Hata siku kadhaa baada ya pambano lake na Banda, Mfaume alitoa taarifa ya kutuomba radhi sisi mashabiki wake akikiri hakucheza vizuri huku akianika sababu huku akiahidi kujifua zaidi.

Kiukweli kijiwe kimefurahishwa sana na ukomavu wa Mfaume Mfaume kwa kuibuka hadharani na kukiri hakucheza vizuri maana sisi wengi tunaujua ubora wake hivyo kwa kile alichokionyesha siku ile alitupunja.

Mwanamichezo wa kwali anapaswa kuwa kama Mfaume kwamba pale anapokuwa hajafanya vizuri anakubali badala ya kutafuta utetezi usio na msingi unaoweza kusababisha watu wakapoteza imani naye.

Lakini, inaonyesha Mfaume ni bondia anayejua namna mashabiki na Watanzania wengi wanavyompa thamani na ndiyo maana hajawachukia baada ya kutofurahishwa na ushindi wake na badala yake amewaomba radhi na kuwaahidi kufanya vizuri baadaye.