Majaliwa anadi maeneo ya uwekezaji, ushirikiano

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amenadi maeneo ya uwekezaji nchini Tanzania alipozungumza na Rais mteule na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Biashara ya Afrika (Afreximbank), Dk George Elombi.

Majaliwa amesema anaamini katika kipindi cha uongozi wa Dk Elombi, benki hiyo itaongeza kwa kiwango kikubwa mchango wake katika kusukuma mbele biashara, maendeleo ya viwanda na uwekezaji wa kimkakati barani Afrika, ikiwamo Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, leo Julai 31, 2025, Majaliwa alihimiza umuhimu wa Afreximbank kukamilisha mpango wake wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha tiba Tanzania, ambacho kitakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa rufaa za nje ya nchi kwa matibabu maalumu.

Waziri Mkuu Majaliwa, ambaye yuko nchini Grenada, ameitaka benki hiyo iendelee kuzingatia utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini, akisisitiza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na miradi yenye tija katika sekta mbalimbali.


“Usaidizi wa kifedha kutoka Afreximbank utaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesema.

Akizungumzia uwekezaji katika uchumi wa buluu, amesema Tanzania ina rasilimali nyingi za baharini ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu.

“Kupitia usaidizi wa Afreximbank, Tanzania inaweza kuendeleza sekta hii kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Vilevile, amezungumzia nishati safi, akisema itakuwa vema endapo benki hiyo itaunga mkono juhudi za matumizi ya nishati mbadala kwa maendeleo endelevu.

“Pamoja na haya, tunaamini Afreximbank itaendelea kupanua wigo wa kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo; benki hii ni mshirika wa kweli katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati unaojali watu wake,” amesema.

Kupitia benki hiyo, amesema Tanzania imenufaika kutokana na msaada wa kifedha na kiufundi kwenye miradi ya Bwawa la Uzalishaji Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACCOP).

Vilevile, kusaidia biashara kupitia benki za Tanzania, sekta binafsi na bajeti za kitaifa kwa kipindi cha 2019 hadi 2024.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa sasa inamiliki hisa 2,323, ambazo ni sawa na asilimia 1.06 ya mtaji wa benki hiyo.

Kwa upande wake, Dk Elombi ameagiza timu ya watendaji wa benki hiyo ihakikishe inakamilisha kwa haraka taratibu zote zinazohusu ujenzi wa kituo cha kisasa cha tiba nchini Tanzania ili mradi huo uanze kutekelezwa na kutoa huduma bora za matibabu ya kibingwa barani Afrika.

Ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuhakikisha fedha zinazotolewa na benki hiyo zinatumika kikamilifu kwa ajili ya miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi, ili malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii yafikiwe.

Amesema ahadi na mikataba yote ya ushirikiano iliyowekwa na mtangulizi wake zitaendelea kutekelezwa kikamilifu.


Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Shariff Ali Sharriff, alisema Tanzania italitumia Jukwaa la Nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (ACTIF2025), lililoratibiwa na Afreximbank, kuimarisha ushirikiano kwenye uchumi wa buluu, ushirikiano maalumu wa taasisi za uwekezaji na za kukuza biashara na sekta za anga na utalii.

Kamishna wa Uchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Fedha, Dk Johnson Nyela, amesema Tanzania na Afreximbank zinaendelea na majadiliano kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Uuzaji Bidhaa Nje Afrika (FEDA), ili kuhakikisha wanatekeleza ujenzi wa kituo cha umahiri wa tiba barani Afrika nchini Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi, Gilead Teri, amesema mamlaka imepanga kujenga kongani ya viwanda kwa kushirikiana na Afreximbank, ambayo imelenga kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini.