MASHABIKI 45 wamenusurika kifo katika ajali ya moto iliyohusisha basi la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) lililokuwa likienda Dar es Salaam, baada ya kuungua kwa moto katika Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.
Ajali hiyo imetokea leo Julai 31, 2025, katika eneo la Bushini, Kata ya Malenve, ambapo gari hilo aina ya Eicher lenye namba za usajili T 284 EFJ lilianza kutoa moshi mkali na baadaye kushika moto, muda mfupi baada ya kuanza safari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, gari hilo lilikuwa limebeba abiria 45 waliokuwa safarini kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kuongeza hamasa kwa timu ya taifa, Taifa Stars itakayofungua fainali za Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika (CHAN 2024).
“Wakati wakiwa safarini, ghafla lilianza kutoa moshi mkali, kisha kushika moto. Hata hivyo, dereva alionesha ujasiri na wepesi kwa kulisimamisha gari kwa haraka na kuhakikisha kila abiria anashuka salama,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa, hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha katika tukio hilo, licha ya gari hilo kuteketea kwa kiwango kikubwa.
Chanzo cha moto huo kinadaiwa ni hitilafu ya mfumo wa umeme wa gari hilo, ingawa uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika.
Aidha, Polisi wamewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kutoa msaada wa haraka uliosaidia kuokoa maisha ya watu waliokuwemo kabla ya vikosi vya Jeshi la Polisi na Zimamoto kufika eneo la tukio.