Rukwa. Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani amelitaka Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia weledi na kulinda taaluma yao badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kutafsiriwa kama upendeleo wa kisiasa.
Aida amesema hayo leo Alhamisi Julai 31, 2025, Mkoa wa Rukwa alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la kukamatwa kwa wanachama 11 wa chama hicho waliokuwa wamekusanyika nyumbani kwake.
Alichokisema Aida kinashabihiana na kilichoelezwa na Ripoti ya Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mifumo ya haki jinai ikiwamo polisi kisha kutoa mapendekezo.
Katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa Rais Samia inaeleza kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi la Polisi.
Malalamiko hayo dhidi ya Jeshi la Polisi yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio.
Hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.
Julai 28, 2025 Polisi Mkoa wa Rukwa iliwakamata wanachama hao wakiwamo viongozi wanne wa chama hicho kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali.
Mbali na kukamatwa kwao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija alimtaka Aida na Alberto Kalilo maarufu Galincha (aliyekuwa diwani wa Itete), kujisalimisha Polisi Wilaya ya Nkasi.
Viongozi waliokamatwa ambao tayari wametoka kwa dhamana ni Winifrida Joseph Khenani (Katibu Mwenezi wa baraza la vijana jimbo la Nkasi kaskazini) na Godfrid Bendera (Katibu wa Chadema Jimbo la Nkasi kaskazini) Evarist Mwanisawa (Katibu baraza la wazee chadema wilaya ya Nkasi) na Scolastica Mwalonde (Mwenyekiti wa chadema kata ya majengo.
Leo Alhamisi, Aida ambaye ubunge wake utakoma Agosti 3, 2025 kwa Tangazo la Rais Samia Suluhu Hassan la kulivunja Bunge ambalo amekwishalitoa amesema takribani robo tatu ya waliokamatwa ni ndugu zake wa karibu.
Amesema ni muhimu kila mmoja, hasa mwenye taaluma kama ya ulinzi na usalama, kuheshimu taaluma yake kwa sababu ndio msingi wa utawala wa haki na amani ya Taifa.
Aidha, mbunge huyo amewataka viongozi wa Serikali na taasisi mbalimbali kuhakikisha uamuzi wao hauna upendeleo wa kisiasa bali uzingatie haki, usawa na masilahi ya Watanzania wote.
“Ni muhimu taaluma ikaheshimiwa ili kila mmoja asimamie majukumu yake ipasavyo, lakini kwa yanayoendelea ni uchochezi na fitina pamoja na upotoshaji,” amesema Aida.
Ameonya kuwa, kiburi cha utawala na matumizi mabaya ya madaraka ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.
Pia, amewataka wananchi wakatae kuyumbishwa kisiasa bali muhimu ni kufanya uamuzi sahihi katika kupata viongozi bora na wapenda maendeleo.
Mmoja wa wanachama wanaodaiwa kukamatwa na jeshi la polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema yeye alikwenda kumtembelea Aida ambaye ni ndugu yake wa karibu.
“Binafsi sielewi kinachoendelea isipokuwa nimejikuta katika adha hii kwa kuwa mimi nilikwenda kumtembelea ndugu yangu,” amesema.
Pia, amelitaka jeshi la polisi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa wana wakamata hata watu wasio na hatia.