Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa ameeleza namna watakavyorahisisha utoaji wa mizigo katika bandari ya Kwala kwenda maeneo tofauti ndani na nje ya nchi, ambao utahusisha uunganishaji reli na bandari.
Mbosa ameeleza hayo alipokuwa akitoa maelezo ya awali kabla ya kuzinduliwa kwa Bandari Kavu ya Kwala uliokwenda sambamba na kupokea mabehewa mapya na yaliyokarabatiwa ya treni ya zamani (MGR), vilivyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Julai 31, 2025.
Bandari hii kwa ujumla ina ukubwa wa hekta 502 ikiwa ni mara tano ya bandari yote ya Dar es Salaam na mpaka sasa eneo lililozungushiwa ukuta ni hekta 60.

Pia sakafu ngumu ikiwa imewekwa kwenye eneo la hekta tano ambalo limeanza kutumiwa likiwa na uwezo wa kutunza kontena 3,500 kwa wakati mmoja ikiwa watapanga kontena tatu kwenda juu na upo uwezekano wa kufika hadi kontena 5,000.
Mbossa amesema wapo hatua za mwisho kuunganisha reli MGR inayotoka Tanga ili iungane na bandari hiyo sambamba na reli ya Tanzania – Zambia (Tazara), ambayo ni kilomita 30 kutoka eneo hilo litakalokuwa likihifadhi mizigo inayotoka bandari ya Dar es Salaam.
Hilo linakwenda kufanyika wakati ambao tayari eneo hilo limeunganishwa na reli ya zamani kutoka Dar es Salaam na Barabara ya Morogoro kwa kilomita 15, ambayo imetengenezwa barabara ya tabaka gumu wakati ambao reli ya kisasa ikiwa mbioni kuunganishwa na bandari ya Bagamoyo.
“Lengo ni mizigo yote ihudumiwe katika eneo hili huku utaratibu wa kuitoa ukifanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) au TPA yenyewe. Hii itasaidia kuwapo kwa mpangilio mzuri wa uondoshaji na upokeaji mizigo,” amesema Mbossa.
Kwa sasa ni treni mbili kwa siku ndiyo zinapokelewa katika bandari hii ambapo kila moja inaweza kubeba kontena 40 na wameanza na zilizokaa muda mrefu bandari ya Dar es Salaam na za kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
“Lengo letu ni kuanza kuchukua kontena zote zinazoshushwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi mbalimbali (transit) na mchakato wa kuzitoa utafanyika hapahapa.”

“Uunganishaji wa reli na bandari utarahisisha harakati za mizigo na kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika soko la kikanda,” amesema Mbossa.
Mbali na wao kama TPA pia wametenga maeneo kwa ajili ya waendesha bandari binafsi (ICD’s), huku wakiweka maeneo maalumu kwa ajili ya mazao ya kilimo na ya kuingiza mizigo kwenye makontena.
Kwa sasa wameanza kufanya kazi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) na mawakala wengine wa Serikali kwa ajili ya kurahisisha utoaji mizigo na hiyo imeanza kwa mizigo ya DRC ambayo unaondokea katika eneo hilo badala ya kuingia bandari ya Dar es Salaam.
Amesema uwepo wa bandari hiyo unapunguza gharama za usafirishaji kwani gari kutoka eneo hilo hadi kupata uwezekano wa kushusha mzigo katika Bandari Kavu ya Dar es salaam inatumia siku nane hadi 14 na hiyo itakuwa imepunguza muda unaotumika.

“Hadi sasa tunaweza kuhudumia kontena 821 kwa siku wakati bandari ya Dar es Salaam inaweza kuhudumia kontena 2,500 kwa siku moja. Pia ili kurahisisha huduma eneo hilo limegawiwa kwa nchi jirani ambazo wanatumia bandari yetu kwa kila nchi kupewa eneo lao,” amesema Mbossa.
Hadi sasa DRC wamepewa mita za mraba 45,000, Zambia 20,000 na wengine 10,000, huku akiweka bayana kuwa upo uwezekano wa kuongezewa maeneo hayo.
“Tayari Burundi wameanza kutengeneza uzio na tunaamini nchi nyingine wataendeleza maeneo waliyopewa ili mizigo yao ihifadhiwe hapo,” amesema.