Samia ataka Kwala imalize foleni Dar

Dar es Salaam. Uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala, iliyoko Kibaha mkoani Pwani, unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa katika kupunguza msongamano wa malori barabarani, kupunguza muda wa safari za usafirishaji wa mizigo na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, hatua inayotarajiwa kuchochea kwa kasi ukuaji wa uchumi nchini.

Bandari hiyo mpya, yenye ukubwa wa hekta 502,  mara tano ya ukubwa wa Bandari ya Dar es Salaam, imezinduliwa sambamba na kongani ya viwanda na mabehewa ya treni ya zamani, huku hekta 60 tayari zikiwa zimezungushiwa ukuta na kuanza kazi rasmi.

Tatizo la foleni, hususan barabara za Morogoro – Mandela hadi bandarini, limekuwa tatizo kubwa. Msongamano huo umekuwa adha kubwa kwa watu kukaa muda mwingi barabarani kutokana na malori kuwa mengi.


Akizungumza katika uzinduzi huo leo Alhamisi, Julai 31, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan amesema uzinduzi wa usafirishaji wa mizigo kwa treni ya kisasa (SGR) hadi Dodoma ni sehemu ya mkakati wa kitaifa kupunguza gharama za usafirishaji, uchakavu wa barabara na kulinda mazingira.

Kwani kwa kutumia reli hiyo, mzigo kutoka bandarini unaweza kufika Kwala kwa dakika 45 hadi saa 1, na Dodoma ndani ya saa 4 hadi 5, tofauti na magari ya mizigo ambayo huchukua wastani wa saa 30 hadi 35

Muda huo ni pamoja na saa 24 hadi 30 za kukamilisha taratibu za kuingia na kutoka bandarini.

“Pia hii inatarajiwa kupunguza msongamano wa malori katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa bandari na kupunguza muda wa ushushaji na usafirishaji wa mizigo,” amesema Rais Samia.

Amesema matarajio yake ni kuona safari hizo zinapunguza gharama za uchukuzi, kuchochea shughuli za kiuchumi ikiwamo viwanda na biashara katika maeneo ambayo magari hayo yatapita, huku ikiongeza ufanisi na mvuto wa Bandari ya Dar es Salaam.

Ili kuimarisha usafiri na usafirishaji wa mizigo, Serikali imewekeza Sh330.2 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 1,430 ya mizigo ya SGR, hivyo aliitaka Wizara ya Uchukuzi na Mammlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha mabehewa hayo yanatumika ipasavyo.

“Shughuli hizi ni za kibiashara, niwasisitize mboreshe vitengo vya biashara na mauzo na kuweka watu wenye weledi na ubunifu kwenye masuala ya biashara. Shirikianeni na wazalishaji wakubwa wa bidhaa mbalimbali waliopo ndani na nje na ukanda wote ili kuvuta mizigo zaidi,” amesema.

Pia amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kushirikiana na reli ya Tanzania–Zambia (Tazara) kama mtoa huduma binafsi, ili kufikia mtandao mkubwa wa mizigo kuhakikisha reli hiyo inatumika kikamilifu.


Pamoja na hayo, ameitaka sekta binafsi kuhamasishwa kuchangamkia fursa hiyo ya kutumia miundombinu ya reli kusafirisha abiria na mizigo kwa kununua vichwa na mabehewa yao.

“Tutoe fursa kwa sekta binafsi wenye uwezo wa ndani na nje ya nchi kuja na mabehewa na vichwa vyao na tukubaliane namna ya kufanya kazi. Sisi Serikali kazi yetu ni kulaza miundombinu, sekta binafsi itumie kufanya biashara, hilo anzeni kufikiria na kuanza mazungumzo,” amesema.

Kufuatia hayo, ameitaka Wizara ya Uchukuzi kukaa na wadau husika ili kuja na mkakati kabambe wa kuondoa msongamano uliopo ili malori yasiyo na sababu ya msingi kuingia Dar es Salaam yaishie Kwala.

“Serikali za mkoa na halmashauri tengeni maeneo ya uwekezaji na msimamie vizuri upangaji wa ardhi na miundombinu rafiki kwa viwanda. Naelekeza hivi kwa sababu ninaona uwepo wa malori mengi hapa Kwala kutalazimu kuimarishwa kwa haraka huduma mbalimbali, ikiwamo za malazi na vyakula,” amesema.

Ili kufanikisha hilo, ameutaka Mkoa wa Pwani kushirikiana na TRA, Wizara ya Uchukuzi kutenga maeneo hayo wakizihusisha kwa karibu wizara za biashara na uwekezaji ili kuhamasisha sekta binafsi kutumia fursa zilizopo.


“Pia niitake Wizara ya Mambo ya Ndani kuimarisha ulinzi katika eneo hili kwa kuweka kituo cha polisi na kufanya doria katika maeneo haya. Miradi tuliyozindua leo itaendelea kuwepo kwa miaka mingi ijayo, hivyo naiagiza TPA na TRC kuwa na mpango wa muda mrefu wa uendelezaji wa eneo hili,” amesema.

Uwepo wa wataalamu toshelevu nao amegusia huku akiitaka Wizara ya Uchukuzi kukamilisha mchakato wa uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Reli kitakachotoa taaluma mahususi za reli na kuimarisha Chuo cha Bandari na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Kuhusu kongani ya viwanda, ametaka viunganishwe na mifumo yote ya usafirishaji ili kurahisisha kupokea na kusafirisha bidhaa zao kutoka Kwala bila kulazimika kwenda nje ya hapo na kuongeza kasi ya kutafuta wawekezaji.

“Pia angalieni gharama za kodi mnazotoza kwa wawekezaji, ardhi ya pale ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi. Angalieni viwango vyenu vya ukodishaji; nadhani ni kikwazo cha wawekezaji wengi kusita kuingia. Pia ni vyema kusimamia sheria zote za uzalishaji Tanzania, ikiwamo ubora wa bidhaa,” amesema.

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliyeshiriki hafla hiyo pia amezungumzia suala la foleni akisema uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala utapunguza msongamano wa kufika Dar es Salaam.

“Nimekuja kwa gari, nikitoka Msoga kuingia mjini napita kwa gari, hayo malori unayopishana nayo ni mengi, ni mengi kupita kiasi. Sasa yale malori yanayokwenda bandarini kuchukua mzigo yatakuja kuchukulia hapa,” amesema.

Amesema hali hiyo itasaidia kuondoa msongamano wa malori kwa watu watakaokuwa wakitoka Pwani kwenda Dar es Salaam na badala yake utaanzia Kwala kurudi nyuma.

Awali, akitoa maelezo kuhusu bandari hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, ameeleza namna watakavyorahisisha utoaji wa mizigo kwenda maeneo tofauti ndani na nje ya nchi kwa kuunganisha reli na bandari.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri wa treni ya umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma eneo la Kwala Marshalling Yard mkoani Pwani, leo Julai 31, 2025.



Mbossa amesema wapo katika hatua za mwisho kuunganisha reli ya MGR inayotoka Tanga ili iungane na bandari hiyo, sambamba na reli ya Tanzania–Zambia (Tazara), ambayo ipo kilomita 30 kutoka eneo hilo litakalokuwa likihifadhi mizigo inayotoka Bandari ya Dar es Salaam.

Hilo linakwenda kufanyika wakati ambao tayari eneo hilo limeunganishwa na reli ya zamani kutoka Dar es Salaam na Barabara ya Morogoro kwa kilomita 15, ambapo imetengenezwa barabara ya tabaka gumu, huku reli ya kisasa ikiwa mbioni kuunganishwa na Bandari ya Bagamoyo.

“Lengo ni mizigo yote ihudumiwe katika eneo hili, huku utaratibu wa kuitoa ukifanywa naTRC au TPA yenyewe. Hii itasaidia kuwapo kwa mpangilio mzuri wa uondoshaji na upokeaji wa mizigo,” amesema Mbossa.

Mbali na wao kama TPA, pia wametenga maeneo kwa ajili ya waendesha bandari binafsi (ICD’s), tofauti na nchi zilizopewa maeneo, huku wakiweka maeneo maalumu kwa ajili ya mazao ya kilimo na maeneo ya kuingiza mizigo kwenye makontena.

Kwa sasa, wameanza kufanya kazi na TRA, Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) na mawakala wengine wa Serikali kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo, na hiyo imeanza kwa mizigo ya DRC, ambayo inaondokea katika eneo hilo badala ya kuingia Bandari ya Dar es Salaam.

“Hadi sasa tunaweza kuhudumia makontena 821 kwa siku, wakati Bandari ya Dar es Salaam inaweza kuhudumia makontena 2,500 kwa siku moja. Pia, ili kurahisisha huduma, eneo hilo limegawiwa kwa nchi jirani ambazo wanatumia bandari yetu, kwa kila nchi kupewa eneo lao,” amesema Mbossa.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema moja ya sababu ya kujengwa kwake ni uwezo mdogo wa bandari kavu zilizokuwapo nchini.

Dar es Salaam ilikuwa na bandari kavu 11 zenye uwezo wa kuhifadhi makasha 24,300, huku bandari kavu za magari zikiwa na uwezo wa kuhifadhi magari 19,100 kwa wakati mmoja, ambazo hazikuwa zinakidhi mahitaji makubwa ya wakati huo na baadaye.

“Sasa bandari hii ya Kwala inatarajia kuhudumia shehena ya makasha yanayokwenda nchi za jirani 823 kwa siku, sawa na makasha 300,395 kwa mwaka, sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam,” amesema.

Amesema bandari hiyo itaongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama na kuimarisha ushindani wa bandari za Tanzania, kuongeza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, na kuchangia katika ongezeko la pato la Taifa.

Katika upande mwingine, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, amesema watahakikisha Tanzania inakuwa nchi kinara katika uzalishaji wa bidhaa ili kupunguza uagizaji kutoka nje, huku ikiongeza uwezo wake wa kuuza bidhaa zake katika masoko ya nje.

Amesema kongani iliyozinduliwa itakuwa na zaidi ya viwanda 200, ikiwa ni uwekezaji wa Dola bilioni 3 za Marekani (Sh7.64 trilioni), ambapo bidhaa za Dola bilioni 6 za Marekani (Sh15.44 trilioni) zitazalishwa, na kati yake bidhaa za Dola bilioni 2 za Marekani (Sh5.09 trilioni) zitakuwa kwa ajili ya kuuzwa nje.