Mavuno hafifu yanayosababishwa na matumizi ya mbolea na viuatilifu bandia, mabadiliko ya ghafla ya mvua, ukosefu wa ujuzi wa kilimo cha kisasa, pamoja na matumizi ya teknolojia zilizopitwa na wakati, ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha uzalishaji wa mazao nchini Tanzania.
Haya ndiyo masuala makuu ambayo mpango wa Serengeti Breweries Limited (SBL) wa ‘Shamba ni Mali’ uliozinduliwa leo unalenga kuyashughulikia, ikiwa ni sehemu ya dhamira mpya ya kampuni kuboresha maisha ya maelfu ya wakulima wa ndani ambao SBL hununua kutoka kwao mahindi, mtama na shayiri yanayotumika katika uzalishaji wa bia.
“Mpango wa ‘Shamba ni Mali’ unalenga kuwanufaisha moja kwa moja zaidi ya wakulima wadogo 4,000 kote nchini, hasa wale wanaolima mtama, shayiri na mahindi. Mpango huu umeundwa kuwawezesha wakulima kwa kuwapatia soko la uhakika la mazao yao, upatikanaji wa mbegu bora zenye tija kwa shayiri na mtama, na mafunzo muhimu juu ya kanuni bora za kilimo, ikiwemo kilimo kinachojali mazingira,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi.
Obinna anaongeza kuwa mpango huo unalenga kuongeza thamani ya biashara kwa kununua malighafi kwa njia endelevu ili kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa wa uhakika, kuimarisha uthabiti na kulinda sifa nzuri ya biashara, huku ukiwahakikishia faida wakulima na kuboresha maisha yao kote nchini.
Mpango wa ‘Shamba ni Mali’ pia utazingatia kujenga uhusiano imara na wakulima kupitia ziara za mara kwa mara za wataalamu kwa ajili ya kubadilishana maarifa na kuendeleza mikutano ya mara kwa mara na wakulima. Kitu kingine muhimu katika mpango huu ni biashara jumuishi, kwa kuwawezesha wanawake, vijana, na makundi yaliyotengwa kwa kushiriki katika mikataba rasmi na kupata huduma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, alisema, “Mpango wa ‘Shamba ni Mali’ unaendana vyema na Mpango Mkuu wa Kilimo Tanzania 2050, wenye maono yanayolenga kubadilisha sekta ya kilimo nchini kuwa endelevu, imara, na jumuishi ifikapo mwaka 2050, na hivyo kuiweka Tanzania kama nchi ya kipato cha kati cha juu.”
Uzinduzi wa mpango huo uliwakutanisha wadau muhimu kutoka Serikalini, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wadau wengine kutoka sekta ya kilimo.
Mwisho
Mkurugenzi Wa Masoko ya Kilimo na Usalama Wa Chakula, Gungu Mibavu (kushoto), akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), Obinna Anyalebechi wakiashiria uzinduzi rasmi wa mradi wa ‘Shamba ni Mali’ wenye lengo la kuwanufaisha wakulima wadogo 4,000 kote nchini, hasa kwa wale wanaolima mtama, shayiri na mahindi. Uzinduzi wa mradi huo wa SBL, uliowakutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini na sekta binafsi, umefanyika mnamo tarehe 31 Julai 2025, jijini Dar es Salaam.