SERIKALI YAWATAKA WAKUU TAASISI ZA UMMA KUTENGENEZA MAZINGIRA RAFIKI YA KAZI

::::::::

Serikali imewataka wakuu wa taasisi za umma kutengeneza mazingira rafiki ya kazi yatakayowawezesha watumishi kuongeza tija na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mhe. Ridhiwani Kikwete, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, alipokuwa akifunga mafunzo elekezi ya siku nne kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali – Kundi la Pili, Jumatano, Julai 30, 2025, katika Shule ya Uongozi ya Mwl. Julius Nyerere, Kibaha, Pwani.

Katika hotuba yake, Waziri Kikwete aliwataka wakuu wa taasisi za umma kusimamia vizuri rasilimaliwatu ikiwa wanataka kuongeza ufanisi wa taasisi wanazoziongoza.

“Ikiwa mnataka kupata matokeo mazuri, mnapaswa kuepuka kuwa miungu watu na badala yake tengenezeni mazingira mazuri ambayo yatawahamasisha watumishi kujituma, kuleta ubunifu na kuongeza tija katika kila ngazi ya utendaji,” alisema Mhe. Kikwete. 

Mhe. Kikwete aliendelea kwa kutoa angalizo, “Lakini simaanishi muwachekee wazembe. Ninachomaanisha ni nyie kufanya kazi kwa msukumo, weledi na kuzingatia misingi ya utawala bora.” 

Hii inamaanisha kuwa wakuu wa taasisi wanapaswa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi anahisi kuheshimiwa na kuwa na nafasi ya kutoa mawazo ambayo yataboresha huduma na kuleta mabadiliko chanya. 

Hii, alisema, ni njia ya kuhakikisha taasisi zinakuwa na tija kwa muda mrefu na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kiutendaji.

Mageuzi yanayoendelea katika kuimarisha utendaji kazi na usimamizi wa Taasisi za Umma yameongeza uwezo wa Serikali kufaidika na uwekezaji wa Sh86.29 trilioni.

Hili linadhihirishwa na gawio la mwaka wa fedha 2024/25, ambapo Mhe. Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan alikabidhiwa Sh1.028 trilioni kama mapato yasiyo ya kikodi kutoka kwa taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.

“Kiasi hicho ni cha kihistoria. Lengo letu la msingi ni kuhakikisha kuwa uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika ya Umma unaendelea kuleta tija kwa Taifa letu kwa mfumo endelevu,” alisema Mhe. Kikwete. 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo, alisema kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina serikali itahakikisha inatengeneza mazingira ambayo yatapelekea kutimia kwa maono ya Mhe. Rais ya kujenga Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali imara na zenye uwezo wa kuharakisha kufikiwa kwa maendeleo ya Taifa letu.

Aidha, Prof Mkumbo alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miongozo ya serikali na sheria zinazohusu usimamizi wa taasisi, kwa lengo la kudhibiti matumizi yasiyo na tija na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma kwa manufaa ya taifa.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi), Bw. Juma Mkomi, alisema mafunzo kwa wakuu wa taasisi, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi ya Uongozi, ni kitendea kazi kikubwa kwani yamegusa rasilimali watu.

Mafunzo hayo yaliyowaleta pamoja wakuu wa taasisi 114 yamewapa washiriki ujuzi na mbinu za kisasa za usimamizi, ikiwemo kuendeleza utamaduni wa uwajibikaji, uwazi, na ufanisi katika taasisi zao.

“Ni imani yangu mafunzo yataongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali watu,” alisema Bw. Mkomi huku akiongeza kuwa, “kujifunza ni suala endelevu, msione haya kujifunza kutoka kwa wasaidizi wenu.”

“Ukijifunza kutoka kwao, wataona na wao ni sehemu ya uendeshaji wa taasisi na hivyo watafanya kazi kwa kujituma na ufanisi Zaidi.”

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema ili kufanikisha safari ya mageuzi ya mashirika ya umma, inahitajika uongozi thabiti, ubunifu, na mshikamano wa pamoja kati ya taasisi za umma, Wizara mama, Ofisi ya Msajili wa Hazina na wadau wengine wa serikali. 

Aliwahimiza watendaji wakuu kuendelea kujifunza na kubadilisha mtazamo wao ili kuendana na mageuzi ya utawala bora yanayohitajika kufanikisha maendeleo endelevu ya taifa.

“Tunaweza kuupata ufanisi wa matokeo chanya kama uongozi utakuwa na ufanisi,” alisema huku akiongeza kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kufanya mageuzi ili taasisi zilete tija iliyokusudiwa.