MSAFARA wa kwanza wa Simba tayari umeshatua kambini jijini Ismailia, Misri, lakini kuna kitu kimefanywa na mabosi wa klabu hiyo kinachoonyesha namna gani walivyopania msimu ujao wa mashindano kwa kuamua kutanguliza majina ya kipa na beki wa kati kambini humo mapema.
Simba iliondoka nchini jana Jumatano kwa msafara wa kwanza ukiwa na baadhi ya nyota waliokuwapo katika kikosi kilichopita na wapya sambamba na watu wa benchi la ufundi, lakini taarifa ya ziada ni kwamba wakati msafara wa pili ukiondoka leo Ijumaa, yamepelekwa kambini majina ya kipa Yakoub Suleiman na beki Wilson Nangu waliopo katika kambi ya timu ya taifa, Taifa Stara inayojiandaa na fainali za Chan 2024.
Nyota hao wawili ni wachezaji waliokuwa JKT Tanzania na inadaiwa tayari wameshasajiliwa na Wekundu hao na mabosi wa klabu hiyo wametanguliza majina yao kambini huko Misri wakati wenyewe wakiendelea kuitumikia Stars iliyopangwa Kundi B la fainali za Chan zinazoanza kesho.
Inadaiwa kuwa, dili la Yakoub Suleiman na Simba limefanyika kimya kimya na wakati wowote lolote linaweza likatokea kwa mchezaji huyo akaibukia Misri katika kambi ya timu hiyo inayoajiandaa na msimu mpya wa mashindano.
Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba mazungumzo ya kumnunua kipa huyo yamefikia pazuri, kilichosalia ni makubaliano ya Simba na viongozi wa JKT Tanzania kutokana na ukweli mchezaji huyo ana mkataba wa miaka miwili na nusu.
Chanzo makini kutoka Simba, kinasema kuwa wakati msimu uliopita unamalizika, kipa huyo alibakiza mkataba wa miezi sita na JKT Tanzania na mabosi wa Yanga walipelekea ofa ya kumsajili kwa Sh100 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini menejimenti yake ilichomoa ikitaka Sh200 milioni.
Hata hivyo, Yanga ilichomoa na ndipo Simba ikaingia mstari wa mbele kumsaka kipa huyo na kufanikiwa kuishawishi menejimenti yake.
“Kipindi hicho Simba ilikuwa haijamfuata Yakoub, alipoona ameshindwana na Yanga akaamua kuongeza mkataba wa miaka miwili na JKT Tanzania, hivyo hadi sasa ana mkataba wa miaka miwili na nusu na timu hiyo ambao Simba wanapaswa kuununua na mazungumzo baina yao yapo pazuri kwa asilimia 80,” kilisema chanzo hicho.
“Yakoub ni askari wa JKU ya Zanzibar, ndio maana ilikuwa ngumu kukubali ofa ya Yanga kwa upande wake isingekuwa na masilahi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Ukiachana na kipa huyo Simba inaendelea kufanya mazungumzo na beki Wilson Nangu ambaye pia inahitaji awe sehemu ya kikosi hicho, kuna mambo yanashughulikiwa ili kila kitu kikae sawa,” kilisema chanzo hicho.
Kuliwepo na taarifa za ndani klabu ya Simba kuachana na kipa mzawa Ally Salim na ilisemekana huenda akajiunga na Namungo, hivyo ikifanikiwa kumsainisha Yakoub atakuwa mbadala wake ambaye kwa sasa yupo na timu ya taifa ya Tanzania, inayojiandaa kucheza michuano ya Chan.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa kwa sasa mabosi wa Simba wanashughulikia viza ya wachezaji hao ili mara baada ya kumaliza majukumu yao na Stars waweze kuungana na wenzao Misri kwani majina yao yameshapelekwa mapema kwa imani JKT haitaleta vikwazo kwa hatua waliyofikia hadi sasa kuwabeba.