Straika Simba anukia Mbeya City

Mbeya City imetuma maombi ya kumuhitaji mshambuliaji wa Simba, Valentino Mashaka baada ya nyota huyo kushindwa kupenya katika kikosi cha kwanza, mbele ya washambuliaji wenzake kikosini humo, Leonel Ateba na Steven Dese Mukwala.

Mashaka aliyejiunga na Simba Julai 5, 2024 akitokea Geita Gold, ameshindwa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha timu hiyo chini ya kocha Fadlu Davids, jambo linaloifanya Mbeya City kuanza kuiwinda saini yake kwa lengo la kuongeza nguvu.

Mwanaspoti linatambua katika mazungumzo yanayoendelea, mabosi wa Mbeya City wanamuhitaji nyota huyo kwa mkopo wa msimu mzima, ambapo Simba imekubaliana na suala hilo, ingawa kilichobakia ni kwa mchezaji wenyewe kufikia makubaliano binafsi.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza mabosi wa Simba wanataka kumtoa Mashaka kwa mkopo kwenda timu itakayompa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwa lengo la kulinda kipaji chake, huku Mbeya City ikiwa ni sehemu sahihi kwake kwenda.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota alisema wachezaji waliokamilisha usajili wao wataweka wazi, ingawa kuna wengine wanaoendelea na mazungumzo nao na watakapokamilisha watawatangaza pia.

Mbali na Mashaka anayewaniwa na Mbeya City, nyota wengine pia waliosajiliwa hadi sasa na kikosi hicho ni mabeki wa kati, Ibrahim Ame aliyetoka Mashujaa, Kelvin Kingu Pemba aliyekuwa Tabora United na kiungo, Omary Chibada wa Kagera Sugar. 

Mbeya City iliyorejea tena Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, tayari imeanza mawindo ya nyota wapya wa kuwaongezea nguvu, ambapo hadi sasa inaendelea na usajili ili kuhakikisha inaongeza ushindani msimu ujao.