Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imetajwa kuchochea ukuaji wa Sekta ya kilimo nchini kupitia mikopo ya pembejeo na zana za kilimo inayotolewa kwa wakulima kote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 31, 2025 jijini Dodoma,mara baada ya kupokea hundi ya mfano ya mdhamini mkuu wa Nanenane Kitaifa yenye thamani ya shilingi milioni 400/zilizotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Jerald Mweli amesema, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo inafanya kazi kubwa ya kuwezesha wakulima kupitia mikopo ya riba nafuu ili kuongeza tija.
“Nanenane ya mwaka huu itaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 10 ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambayo imefanya kazi kubwa ya kuleta mageuzi katika Sekta ya kilimo,” alisisitiza Mweli.
Akieleza zaidi, Bw. Mweli amesema wakati wa maonesho hayo kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano,huduma kutoka taasisi za kifedha kwa wakulima na elimu kwa wakulima itatolewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw.Frank Nyabundege amesema utashi wa kisiasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan umeiwezesha Benki hiyo kuwa miongoni mwa benki kubwa hapa nchini.
Alieleza kuwa,Sekta ya kilimo imeajiri zaidi ya asilimia 70 ya watanzania, hivyo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
“Benki ya Maendeleo yaKilimo ni kinara katika utoaji wa mikopo katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuongeza tija na inashirikiana na benki 19 katika kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima kwa dhamira ya kukuza sekta ya kilimo”, alisisitiza Nyabundege
Akitaja mafanikio ya Benki hiyo amesema ni pamoja na kuongezeka kwa ukubwa wa benki hiyo na kufikia thamani ya shlingi trilioni 1.2 kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita tangu ilipoingia madarakani mwaka 2021.
Kuhusu mikopo iliyotolewa na Taasisi za fedha kwa sekta ya kilimo Bw.Nyabundenge amesema imefikia zaidi ya shilingi trilioni 4 katika kipindi cha Rais Samia Suluhu Hassan.