SAA 48 kabla ya fainali za Ubingwa wa Nchi za Afrika (CHAN) 2024 kuanza rasmi kwa mechi ya ufunguzi itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua kampeni maalumu ya fainali hizo zitakazomalizika Agosti 20.
Fainali hizo za nane zinazofanyika kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki ikiandaliwa na Tanzania, Kenya na Uganda, inashirikisha jumla ya nchi 19 wakiwamo watetezi, Senegal waliopangwa Kundi ambalo mechi zao zinafanyika visiwani Zanzibar.
Katika kuleta hamasa kwa fainali hizo kubwa zikifanyika Tanzania, Bosi ya Utalii imezindua kampeni maalumu ya ‘Tinga Chan, Tinga Tanzania’, ambapo Mkurugenzi wa bodi hiyo, Ephraim Balozi Mafuru amesema wanatarajia kutumia fulsa ya uwenyeji wa mashindano CHAN, kuvutia watalii kutembelea nchi hususani kupitia zao la utalii wa michezo ambao ni moja ya mazao ya utalii yanayokua kwa kasi.
Mafuru alisema kampeni ya Tinga Chan, Tinga Tanzania inalenga kuchochea ongezeko la watalii wa ndani na kimataifa sio tu wakati wa fainali hizo za CHAN bali hata baada ya mashindano hayo kwa kuvitangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini kupitia matangazo yatakayorushwa CHAN 2024.
“Tutahusisha ziara maalum za kutembelea vivutio vya utalii ili kutoa fursa kwa wageni waliokuja nchini sanjari na wananchi wa Tanzania kufurahia rasilimali zetu za utalii, kadhalika, yatakuwepo matukio mengine yenye muktadha wa kitalii kama vile mikusanyiko ya kutazama mechi itakayoambatana na burudani mbalimbali;

“Ni fursa ya kutangaza vivutio vyetu kwa wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanaoshiriki mashindano hayo. Vilevile, ni fursa ya kuendelea kudhihirisha ubora wa nchi yetu katika utalii ambapo mtakumbuka kuwa hivi karibuni tulishinda Tuzo mashuhuri za utalii ikiwemo kivutio bora cha Utalii Barani Afrika (Africa’s Leading Destination) na Kivutio Bora cha Utalii wa Safari Duniani (World’s Leading Safari Destination),” alisema Mafuru na kuongeza;
“Kama mnvyofahamu, Tanzania imepewa heshima ya kuwa mojawapo ya waandaaji wa mashindano ya CHAN 2024, mashindano hayo yanafanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka huu ambapo jumla ya nchi 19 za Bara la Afrika zimethibitisha kushiriki.
Nchi hizo ni pamoja na Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika Kati, Senegal, Jamhuri ya Congo, Sudan, Nigeria, Uganda, Niger, Guinea, Algeria, Afrika Kusini, Kenya, Morocco, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Zambia.
Alisema Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ni fursa adhimu ya kuvutia watalii kutembelea nchi hususani kupitia zao la utalii wa michezo ambalo ni mojawapo ya mazao ya utalii yanayokua kwa kasi duniani.
“Ni fursa ya kuendelea kudhihirisha ubora wa Nchi yetu katika utalii ambapo mtakumbuka kuwa hivi karibuni tulishinda Tuzo mashuhuri za utalii ikiwemo Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (Africa’s Leading Destination) na Kivutio Bora cha Utalii wa Safari Duniani (World’s Leading Safari Destination).

Alisema ni matarajio yao, kampeni ya Tinga CHAN, Tinga Tanzania itachochea ongezeko la watalii wa ndani na kimataifa sio tu wakati wa Mashindano ya CHAN bali hata baada ya mashindano hayo. Hiyo ni kutokana na hamasa itakayojengeka kupitia matukio na shughuli za utangazaji utalii zitakazofanyika.
“Kwa usuli huo, napenda kutoa rai kwa wadau wa utalii hapa nchini kuchangamkia fursa za utalii zitakazotokana na Mashindano ya CHAN 2024 ikiwemo huduma za malazi, vyakula, usafiri, burudani, uratibu wa safari za utalii, na nyinginezo. Kwa upande wetu, Bodi ya Utalii tumejipanga vema kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha tunanufaika na fursa tajwa.” alisema Mafuru.