Tucasa yataja mwarobaini ucheleweshaji malipo ya makandarasi

Dar es Salaam. Ili kukabiliana na changamoto ya ucheleweshaji wa malipo ya makandarasi, Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (Tucasa) kimependekeza kuanzishwa kwa sheria ya malipo (Security of Payment Act).

Pia wamependekeza taasisi za ununuzi kutoa dhamana ya malipo (Payment Guarantee) ili kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa malipo.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Julai 31, 2025 na msemaji wa chama hicho, Harris Kapiga katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Kapiga amesema anaamini itasaidia makandarasi kupata malipo yao kwa wakati ili kuweza kutekeleza miradi yao kwa ufanisi zaidi.

Amesema ucheleweshwaji wa malipo kwa makandarasi na watoa huduma shirikishi ni moja ya kikwazo kinachozorotesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na sekta ya ujenzi kwa ujumla.

Pia amesema inaathiri maisha ya makandarasi, wafanyakazi, wasambazaji na uchumi kwa ujumla.

“Makandarasi wengi wanakumbwa na hali ngumu ya kifedha, kupoteza ajira, kushindwa kukamilisha miradi kwa wakati na wengine hata kukata tamaa na kuchukua hatua hatarishi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Tucasa, Samuel Marwa amesema kukiwa na sheria ya malipo itakuwa na manufaa kwa pande zote mbili yaani Serikali pamoja na makandarasi.

Marwa amesema kwa upande wa mkandarasi itamhakikishia kupata malipo yake kwa wakati hivyo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Pia amesema mkandarasi anapokuwa na uhakika wa malipo hata gharama ya utekelezaji wa mradi husika huwa nafuu.

Amesema hata uzoefu kutoka nchi mbalimbali zilizoanza kutumia sheria hiyo bei za soko zilishuka.

“Hivyo bei za soko zinaposhuka Serikali inaweza kutekeleza miradi mingi zaidi,” amesema.

Awali, Kapiga amesema suala hilo pia wanatarajia kulijadili kwa kina katika mkutano wao wa mwaka unaotarajiwa kufanyika Septemba 2-3, 2025 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na makandarasi takriban 1,000.

“Pamoja na mambo mengine wataalamu hao watajadili kwa kina ni kwa namna gani watakwenda kuboresha sekta ya ujenzi, huku tukitarajia mgeni rasmi kuwa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.