KESHOKUTWA ndiyo siku muhimu na kubwa katika soka letu hapa Tanzania ambalo ni mechi ya ufunguzi wa Fainali za CHAN baina ya Taifa Stars na Burkina Faso pale katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Sisi hapa kijiweni tumefurahia sana kusikia mechi hiyo imepangwa kuchezwa kuanzia saa 2:00 usiku kwa sababu tunaamini ni muda sahihi ambao watu watakuwa wameshatoka makazini na katika shughuli nyinginezo na kwenda uwanjani.
Tuna kila sababu ya kuiunga mkono timu yetu ya taifa kwa vile sapoti yetu mashabiki ina nafasi kubwa sana katika kuwahamasisha wachezaji wetu wapiganie bendera ya Taifa.
Hii ni timu yetu ya taifa na hakuna nyingine zaidi ya hiyo, hivyo tusipoisapoti sisi tusitegemee kuna watu kutoka nchi nyingine watakuja kufanya hiyo kazi ambayo sisi itakuwa imetushinda.
Kwa kuanzia hapa kijiweni tumekubaliana tuweke kando itikadi zetu za klabu na kuungana kwenda Benjamin Mkapa na hili tutalifanya kipindi chote cha mashindano.
Hakuna sababu ya kuitenga timu ya taifa kwa sasa maana ndiyo alama ya nchi yetu na ndiyo inatuunganisha na kuthibitisha hilo, ni lazima wimbo wa taifa utapigwa kabla ya mechi kuchezwa.
Kama kuna changamoto na kutofautiana kokote ambako kumewahi kutokea siku za nyuma basi tujitahidi kuuweka kando kwa muda na kuwa kitu kimoja kuhakikisha chama letu linatoboa CHAN.
Itakuwa ni jambo la kushangaza kuona mashindano makubwa kama haya yanafanyika katika nchi yetu na sisi wenyeji tunaitenga timu yetu ya taifa na hatujitokezi uwanjani.
Tuna imani tukifurika pale Kwa Mkapa, wachezaji wetu watapata nguvu na morali ya juu ambayo itaifanya Burkina Faso iziache pointi zote tatu pale.