WAGOMBEA JUMUIYA YA WAZAZI JIEPISHENI NA RUSHWA

:::::::::

Katibu mkuu Jumuiya ya wazazi wa chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi ‎amewataka wagombea wa ubunge viti maalumu kupitia jumuiya hiyo pamoja na wapambe wao kuzingatia kanuni na Sheria za uchaguzi wa chama hicho na kujiepusha na masuala yote yatakayotia dosari uaminifu wao kwenye chama ikiwemo vitendo vya rushwa.

Hapi ameyasema hayo leo Julai 31,2025 Jijini hapa Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano mkuu maalum wa Jumuiya hiyo utakao fanyika kesho Agosti Mosi katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete ili kufanya uchaguzi wa wabunge wa viti maalum na wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wa Jumuiya hiyo.

Aidha, amewataka wagombea wote kujiepusha na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi huo ili watakaochaguliwa watokane na sifa zao na siyo kwa kutumia rushwa kwani chama pamoja na vyombo vya dola havitawafumbia macho watu wa aina hiyo.

“Wale ambao watashindwa kwenye uchaguzi huu naomba muendelee kuwa watulivu ndani ya chama kwani nafasi zinazogombaniwa ni chache hivyo kuna watakaopata na wengine watakosa kwa sababu siyo kila mtu atapata,”amesema. 

Mbali na hilo amesema mkutano mkuu maalumu wa jumuiya hiyo utawakutanisha jumla ya wajumbe 756 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kufanya uchaguzi wa wagombea hao.

 “Jumla ya wagombea 19 watachuana ili kupata wagombea wawili wa ubunge na wagombea wawili wa Baraza la wawakilishi Zanzibar,”amesema. 

Amesema ili kupata nafasi hizo jumla ya wagombea 60 walichukua fomu huku upande wa Tanzania Bara pekee wakiwa wagombea 33 ambapo jumla ya majina ya wagombea 19 yalipitishwa na Kamati kuu.

“Kwa hiyo tutakuwa na wagombea 19 wa ubunge Bara, tutakuwa na wagombea nane wa nafasi ya uwakilishi Zanzibar na tutakuwa na wagombea sita watakaogombea kiti cha ubunge wa viti maalum kwa upande wa Zanzibar, jumla tunao watu 33 watakaoingia kwenye mchuano wa kinyang’anyiro cha kesho,” amesema Ali Hapi