Dar es Salaam. Wakazi watatu wa Kyela mkoani Mbeya wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 51 yakiwemo ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na kujipatia Sh1.8 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Wakili wa Serikali, Michael Sindai amewataja majina yao ni Daniel Mwazyele (20), Athuman Mwakoko (21) na Obadia Mwakwenda (22).
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga.
Wakili Shindai amedai kati ya mashtaka hayo 51, 24 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, 22 ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa majina ya mtu mwingine, matatu ya kusambaza taarifa za uongo, moja ya kutakatisha fedha na lingine ni kuongoza genge la uhalifu.
Akiwasomea mashtaka yao, wakili Shindai amedai katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu washtakiwa wanadaiwa
kutenda kosa hilo kati ya Mei 10,2025 na Juni 10, 2025 washtakiwa wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliongoza genge la uhalifu kwa kuchapisha taarifa za uongo na kujipatia Sh1.8 milioni kutoka kwa watu tofauti.
Washtakiwa katika tarehe hizo wanadaiwa walituma ujumbe mfupi wa maneno katika laini za simu za watu mbalimbali wakiomba pesa, huku wakijua ni kinyume cha sheria.
Pia katika kipindi hicho, washtakiwa wanatuhumiwa kutumia laini za simu zilisajiliwa kwa majina ya watu wengine bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na kujipatia Sh1.8 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Katika shtaka la utakatishaji fedha, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2025 hadi Februari 10, 2025 walijipatia Sh1,8 milioni, huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Ruboroga aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.