INAELEZWA huenda Yanga Princess ikakamilisha usajili wa beki wa kati raia wa Nigeria, Akudo Ogbonna, akitokea IFK Kaimal inayoshiriki Ligi Kuu nchini Sweden.
Mbali na Akudo, lakini inaelezwa Yanga Princess imemalizana na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Precious Christopher na Ritticia Nabbosa.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo alisema tayari amesaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza kama atafanya vizuri.
“Ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga walikuwa wamemfuatilia kwa takribani miaka miwili, wamefanikiwa kwa sasa,” alisema mtu huyo.
Kama atacheza Yanga msimu ujao, huenda akakutana na ushindani kwenye eneo hilo ambalo wamekuwa wakicheza Wanigeria wenzake, Igwe Uzoamaka na Angela Chineneri, waliosajiliwa msimu uliopita na wakicheza kwa maelewano makubwa.
Miongoni mwa mafanikio ya beki huyo ni pamoja na kunyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi (WAFCON) mwaka 2022, Beki Bora wa Ligi ya Sweden (2024), na Beki Bora wa Ligi Kuu Nigeria (2023).