Zanzibar yajipanga kuongeza ufaulu elimu ya msingi

Unguja. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikitekeleza mageuzi ya elimu, imeingia makubaliano na shirika binafsi la Room to Read kutekeleza mradi wa usomaji na maktaba kusaidia kuongeza ubora wa elimu ngazi ya msingi.

Makubaliano hayo yameingiwa kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na shirika hilo, yakilenga kuongeza kiwango cha K3 (kusoma, kuandika na kuhesabu). Pia yanahusu mradi wa usawa wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo leo, Julai 31, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdulla Said, amesema ushirikiano huo unakwenda kuinua stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ambazo ndizo msingi mkuu wa elimu duniani.

“Tunataka kupindua meza kwenye matokeo, kuongeza ufaulu katika mitihani. Tutashirikiana kujenga uwezo wa walimu kwa kushirikiana na wafanyakazi wa maktaba kuangazia hasa maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa ili kuleta mageuzi katika sekta ya elimu,” amesema.

Ametaka kuanzishwa vitu vipya kupitia mradi huo kwa kufanya tathmini ya maeneo yenye uhitaji zaidi na kuongeza nguvu.

Khamis amesema iwapo watafanya vizuri, Zanzibar itakuwa na wataalamu wengi watakaofanya kazi ndani na nje ya nchi kutokana na misingi ambayo itakuwa imejengwa tangu awali.

Amesema kwa sasa ufaulu katika elimu ya msingi kwa maana ya alama A mpaka D upo wastani wa asilimia 89.

“Mradi huu unakuja katika muda sahihi wa kutekeleza mageuzi ya elimu, Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, Ajenda ya Afrika Tuitakayo na mipango ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo hiki kinachofanyika kinakwenda kutimiza malengo hayo kwa asilimia 100,” amesema.

Licha ya kazi hiyo kuwa jukumu la Serikali, amesema wametengeneza sera za kukaribisha sekta binafsi na asasi nyingine kutekeleza haya kwa ufanisi.

Kutokana na jitihada zinazochukuliwa, amesema itakuwa fursa ya kuwapima walimu, na wale watakaofanya vizuri watapewa motisha, huku hatua kwa watakaofanya vibaya zitachukuliwa. Lengo likiwa si kukomoa bali kuhamasisha utendaji kazi uliotukuka

Hatua hiyo, amesema, italeta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu ambayo ndiyo msingi mkuu wa uchumi wa Taifa lolote duniani.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read, Joan Minja, amesema kuna vifaa vya kujifunzia na kuboresha mazingira ya ujifunzaji kupitia maktaba shuleni.

Kupitia mradi wa usawa wa kijinsia, amesema wataendeleza juhudi za kuwawezesha wasichana na wavulana katika shule za msingi na sekondari kwa kuwajengea stadi ili kutatua changamoto zinazowakabili na kufanikiwa kuhitimu masomo yao.

“Room to Read tunaamini mabadiliko ya ulimwengu huanza na watoto walioelimika, hivyo kila mtoto, mvulana na msichana ana haki sawa kupata elimu bora na kufikia ndoto zake katika maisha. Hatua hii ni muhimu kufikia utekelezaji wa mpango mkakati wa kufikia watoto wengi na haraka zaidi,” amesema.

Amesema wamedhamiria kuongeza kasi ya kuboresha matokeo kwa kushirikiana na walimu, wazazi na jamii zote Zanzibar.