Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Jiji hilo linatumia megawati 678 za umeme uliopo kwenye gridi ya Taifa kiwango ambacho ni sawa na asilimia 16.8 ya umeme wote uliokuwa unazalishwa hadi Aprili mwaka huu.
Kwa sasa mahitaji ya juu ya umeme katika Gridi ya Taifa nchini yameendelea kuongezeka na kufikia Megawati 1,921.44 zilizofikiwa Aprili, 2025 ikilinganishwa na megawati 1,590.10 zilizofikiwa Machi, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 20.84.
Chalamila ameyasema hayo wakati wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akifungua Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) Ubungo Dar es Salaam, leo Ijumaa, Agosti 1, 2025.
Amesema awali kulikuwa na wasiwasi kwa baadhi ya wawekezaji katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kuwa umeme utakuwa changamoto.
“Wakati wale wapangaji 400 wakiwa wamefika hapa walionyesha wasiwasi wao, kwanza kuhusu umeme katika kituo hiki kama unaweza kuwa rafiki. Kituo hiki, kinatumia megawati 1.7 kwa sasa lakini wapangaji wote wakiingia kitatumia megawati 4.
“Kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam, tunatumia megawati 678 haya ni matumizi ya juu kabisa kuliko Mkoa wowote Tanzania,” amesema.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa sasa Dar es Salaam ina miradi minne inayoendelea kujengwa, ikiwemo njia ya kusafirishia umeme wa kilovoti 220, vituo vya kupoozea umeme Ununio na Mabibo vinavyotengenezwa kwa zaidi ya Sh250 bilioni.
“Rais hili tulilileta kwako kwamba ukuaji wa uwekezaji unaongezeka, tunahitaji umeme himilivu naomba niwatoe mashaka wanaofanya uwekezaji, Tanesco wamejipanga na tunawathibitishia umeme hautakuwa tatizo kwa Dar es Salaam,” amesema.
Chalamila amesema miradi mingine ya ujenzi wa njia za barabara za mwendokasi unaendelea ikiwemo njia inayojengwa kwa gharama ya Sh235 bilioni kwa ajili ya kuleta wanunuzi na wafanyabiashara kwenye kituo hicho.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida amesema kituo hicho kina jumla maduka 2,060 na mpaka wakati huu wa ufunguzi tayari kuna wafanyabiashara zaidi ya 400 waliopo hapo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Tiseza), Gilead Teri amesema mamlaka hiyo itaboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Kupitia uwekezaji wa kituo hicho, utazalisha ajira 15,000 za moja kwa moja na ajira zisizo za moja kwa moja 50,000, vizimba 2060, na kitaleta faida ya zaidi ya Sh400 bilioni na kila mwaka kwa fedha za kigeni zaidi ya bilioni 25 kama mapato ya serikali, kwamba hiyo ni nje ya mapato mengine kama VAT ambayo TRA itakusanya kila mwaka.
“Tangu Julai Mosi Tiseza imekuwa ikiendelea na jukumu la usajili. Jumla ya miradi 503 imeletwa nchini yenye thamani ya Dola za Marekani 5.9 bilioni na katika miradi hii Watanzania 107 na wageni 244 na wabia 101. Wizara imetupa lengo la miradi 1500 ifikapo Desemba mwaka huu,” amesema Teri.