BOLT NA TODA YAENDESHA MAFUNZO YA SIKU 10 KWA MADEREVA JIJINI DAR ES SALAAM

::::::::

 Kampuni ya usafiri wa mtandaoni Bolt Tanzania, kwa kushirikiana na Chama cha Madereva Mtandaoni Tanzania (TODA), imezindua mafunzo ya siku 10 kwa madereva wake wa jijini Dar es Salaam.

Programu hiyo inahusisha vipengele vitatu muhimu, ikiwemo mafunzo na vyeti vya Usafiri wa Umma (PSV) kwa ushirikiano na Taasisi ya Usafirishaji Tanzania (NIT), Moduli ya Bolt Best Practices inayolenga kuongeza huduma bora na kujenga uhusiano wa heshima kati ya dereva na abiria, pamoja na mafunzo ya misingi ya kukabiliana na dharura barabarani ili kuwajengea madereva uwezo wa kushughulikia matukio kwa haraka na kwa usalama.

Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Tanzania, amesema mpango huo unaonesha dhamira ya kampuni katika kuhakikisha usalama, utiifu wa sheria na uwezeshaji wa madereva nchini, “Kupitia mafunzo haya, madereva wanapata fursa ya kueleza changamoto zao na kujifunza mbinu bora za kushughulika na abiria wasumbufu pamoja na matukio yasiyotarajiwa barabarani,” alisema.

Kanyankole aliongeza kuwa matokeo ya tafiti za hivi karibuni yanaonesha abiria huangalia zaidi heshima na weledi wa madereva kama kigezo cha kuchagua huduma za usafiri wa mtandaoni. Alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya abiria huzingatia tabia na weledi wa dereva kama kigezo cha uaminifu na kurudia kutumia huduma husika.

Bolt imesisitiza kuwa itaendelea kuwekeza katika mafunzo ya aina hii ili kuongeza taaluma za madereva, kuboresha ubora wa huduma na kuongeza kuridhika kwa wateja. Hatua hii pia inalenga kusaidia madereva kuzingatia sheria za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kukuza maendeleo ya sekta ya usafiri wa mtandaoni nchini.