Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amefungua maonyesho na sherehe za wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) akisisitiza mambo manane, hawa kwa viongozi wa sasa na watakaochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba.
Ufunguzi huo umefanyika kitaifa leo Agosti Mosi, 2025 katika Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma, ikiwa na kaulimbiu isemayo: “Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi 2025.”
Kaulimbiu hiyo ni mahususi kuwakumbusha wananchi umuhimu wa viongozi bora katika kuinua uzalishaji kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika hotuba yake, Dk Mpango amesema jambo la kwanza ni wajibu wa viongozi kutekeleza Dira ya 2050 na mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo inayotaka kuongeza kasi ya ukuaji wa kilimo hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030 na kuendelea.
“Hivyo, viongozi tuna wajibu wa kuhakikisha tunaifanya Tanzania kuwa kitovu cha chakula katika ukanda wa Afrika na kusimamia mageuzi yanayohitajika kufikia malengo hayo. Pamoja na mambo mengine, tunawajibika kuwaelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi kuweka nguvu zaidi kwenye mazao yenye thamani kubwa sokoni,” amesema.
Mbali ya hayo, amesema wanapaswa kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa wa bidhaa zinazotokana na mifugo ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje, kuendeleza uvuvi na ufugaji wa samaki na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje na kuwekeza katika miundombinu baridi ya uhifadhi na usafirishaji.
Pia amesisitiza kujiimarisha zaidi katika kilimo-biashara, kuhamasisha uwekezaji mkubwa katika teknolojia za kisasa za kilimo, ikiwemo kilimo-janja, uwekezaji katika umwagiliaji, upatikanaji wa fedha na mitaji na kutafuta masoko ya uhakika.
Jambo la pili amesema viongozi wanahimizwa kusimamia uwezeshaji wa wakulima, wafugaji na wavuvi kiuchumi, hususani upatikanaji wa mitaji, teknolojia, elimu na mafunzo. Vilevile upatikanaji wa huduma za ugani, ikiwemo kukuza matumizi ya kanuni bora za kilimo.

Tatu, wahamasishe maendeleo ya ushirika na ushirikiano kati ya wakulima, wafugaji, wavuvi na watafiti, maofisa ugani na watunga sera.
“Jambo hili litawezesha kubadilishana na kuchangiana elimu/ujuzi, rasilimali, mbinu bora na mifano halisi ya kuongeza tija,” amesema.
Jambo la nne ni wajibu wa kuhimiza utekelezaji wa sera na mikakati inayowezesha kilimo kukua kwa haraka zaidi, hususani uwekezaji katika miundombinu wezeshi, utafiti na elimu. Pia, utekelezaji wa sera zinazowezesha kilimo-biashara ili kutengeneza faida na kumlinda mkulima.
Tano, amesema wana wajibu wa kuhimiza wananchi kutumia mbinu zinazoweza kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na changamoto nyingine zinazowakumba wakulima.
“Hii ni pamoja na kuhimiza matumizi bora ya ardhi, kushawishi wananchi kupanua mawanda ya kilimo na kuhimiza zaidi kilimo cha mazao yanayohimili ukame,” amesema.
Sita, amesema ni kuweka mkazo katika kujenga nguvukazi na rasilimali watu yenye ubora kwa maendeleo ya kilimo, kwa kutilia mkazo mafunzo kwa vitendo kwa wakulima na wataalamu wa kilimo. Pia kujenga na kuendeleza taasisi za kilimo, zikiwamo ushirika na vyama vya wakulima.
Jambo la saba, amesema ni kufuatilia na kupima matokeo ya utekelezaji wa mipango na miradi ya kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Tumieni matokeo ya ufuatiliaji na tathmini kuelekeza rasilimali ili zitumike kwa tija zaidi na kufikia malengo,” amesema.
Nane, amesema ni wajibu wa kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhusu fursa zilizopo za kupata mitaji kutoka benki na taasisi nyingine za fedha ambazo tayari zinatoa mikopo nafuu kwa ajili ya kilimo-biashara.
Pia kuwaunganisha na kampuni za teknolojia, vyuo vikuu na taasisi za ufundi zinazobuni teknolojia rahisi na nafuu, zikiwemo za kuchakata na kuhifadhi mazao kwa ajili ya kuongeza tija katika sekta hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza vipaumbele vya kilimo, ikiwamo kuongeza tija za uzalishaji, kuchangia kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo.
Pia kuimarisha usalama wa chakula na lishe, upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi.
Vilevile, kuimarisha maendeleo ya ushirika na matumizi ya mifumo ya Tehama katika uendelezaji wa sekta ya Kilimo.
Amesema wizara imeendelea kuwashauri, kuwaelimisha na kuwawezesha wakulima kuzingatia sheria na maelekezo ya wataalamu ya kutunza mazingira, kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti na kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia za kilimo.