Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC), Dk Lisa Wang amesema Kituo hicho kitawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kupanua biashara zao kikanda na kimataifa.
Ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kufungua rasmi kituo hicho iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan leo, Agosti Mosi 2025.
Kituo hicho kimegharimu Sh282.7 bilioni hadi sasa, huku ujenzi wake ukijumuisha jumla ya sehemu 2,060 za maduka na ofisi. Mradi unatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 15,000 za moja kwa moja na ajira zisizo rasmi 50,000.
Amesema lengo lao ni kukuza biashara ya pande zote mbili huku akisema kwa sasa wanasafirisha mazao ya Tanzania kama soya, kahawa, ufuta na korosho kwenda China.
“Tunajivunia kuwa kampuni ya kwanza kusafirisha bidhaa bora na za asili kutoka Tanzania kama vile kahawa na asali kwenye soko la China wakati ambao sisi tunaagiza bidhaa muhimu kama vile mashine na bidhaa za matumizi ya kila siku,” amesema.
Amesema kituo hicho mradi tu, bali ni ahadi inayojenga mfumo wa kisasa wa biashara unaohudumia kanda na kuinua maisha ya watu wake.
“Mheshimiwa Rais, tunakuhakikishia kuwa Kituo hiki cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki kitaleta ajira, fursa na mapato kwa taifa,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo kuhusu Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo Jijini Dar es Salaam leo Agosti 1, 2025.
Amesema kituo hicho ni kikubwa zaidi cha biashara na usafirishaji nchini Tanzania huku kikiwa kimeunganishwa na huduma za forodha, biashara ya mtandaoni, minyororo ya usambazaji.
“Mradi huu utapunguza gharama za biashara kwa kiwango kikubwa, kutengeneza ajira mpya na kuongeza mapato ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa,” amesema Dk Lisa.
Amesema tangu kuanza kwake, EACLC tayari imechangia zaidi ya Sh22 bilioni na wamejizatiti kuongeza mchango huo kwa kiwango kikubwa katika siku zijazo.
“Tupo hapa kuongeza thamani katika masoko ya ndani kwa kuleta bidhaa za kimataifa, kuvutia wateja wapya na kuruhusu wafanyabiashara wa ndani kufaidika na miundombinu ya kisasa ya kimataifa. Tunawaalika wafanyabiashara wa Tanzania kushirikiana nasi na kukua pamoja,” amesema.
Amesema wanaamini kuwa EACLC itakuwa kitovu cha viwanda na biashara za kikanda Kupitia eneo la biashara huru la Afrika (AfCFTA) ambapo Tanzania ni sehemu ya jumuiya hiyo.
“Tunalenga kuvutia wazalishaji wa kimataifa kuanzisha viwanda vya usindikaji na uunganishaji hapa Tanzania kwa ajili ya soko la ndani, Afrika Mashariki na hata zaidi,” amesema.
Amesema Kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam, EACLC wanatengeneza jukwaa la huduma zote, linalojumuisha Kituo cha Biashara na Usafirishaji, ghala la kimataifa la Tanzania, Kituo cha Maonyesho ya Kimataifa, eneo maalumu la usafirishaji, kitovu cha mizigo kupitia uwanja wa ndege, na jukwaa la biashara mtandaoni baina ya nchi.
“Hii ina maana kwamba bidhaa za Tanzania kama kahawa ya Kilimanjaro, korosho na karafuu za Zanzibar hazitangoja tena fursa zitaifikia dunia moja kwa moja,” amesema.
Amesema huo ni ushuhuda kuwa EACLC imejipanga kuwekeza zaidi hapa Tanzania na watawagusa zaidi vijana na wanawake.
“Hii ni kwa sababu tunaunga mkono ajenda yako ya viwanda, tutafungua njia mpya ya usafirishaji, kupunguza muda wa upokeaji mizigo kutoka China kwa takribani nusu, kutoa huduma za kuuza bidhaa nje kwa zaidi ya biashara ndogo na za kati na kuanzisha mifumo mipya ya usafirishaji itakayoongeza mara mbili ufanisi wa usambazaji,” amesema.
Mbaki na biashara amesema wanatekeleza programu za mafunzo za kina ili kulea kizazi kipya cha Watanzania wenye ujuzi katika usafirishaji, biashara mtandaoni na usimamizi.
“Mama Samia, uliwahi kusema kuwa “Ustawi wa Afrika ni lazima uongozwe na Waafrika.” Maneno haya tumeyachukua kwa uzito mkubwa. EACLC tayari imefikia asilimia 93 ya utekelezaji kwa kutumia wataalamu na rasilimali za ndani. Tupo hapa kama washirika si kama watawala tupo kuwezesha si kuchukua nafasi tupo kushirikiana si kuchukua nafasi ya mtu yeyote,” amesema.