Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakati akiweka jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda ya Kwala, Mkoani Pwani, kwa ajili ya ujenzi wa viwanda 200 vya kisasa ambapo TANESCO, kupitia Kampuni Tanzu ya ETDCO, tayari imekamilisha ujenzi wa njia ya kusambaza umeme ya msongo wa kilovolti 33 yenye urefu wa kilomita 18 katika eneo hilo ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Dismas Massawe (katikati) akizungumza jambo na wadau katika hafla ya kuweka jiwe la msingi Kongani ya Viwanda ya Kwala, Mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
……….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda ya Kwala, mkoani Pwani, kwa ajili ya ujenzi wa viwanda 200 vya kisasa ambapo TANESCO, kupitia Kampuni Tanzu ya ETDCO, tayari imekamilisha ujenzi wa njia ya kusambaza umeme ya msongo wa kilovolti 33 yenye urefu wa kilomita 18 katika eneo hilo ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana.
Akizungumza katika hafla ya kuweka jiwe la msingi iliyofanyika Julai 31,2025 Mkoani Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazalo Twange, amesema kuwa TANESCO kupitia ETDCO imefanikiwa kutekeleza mradi huo kama sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu rafiki kwa maendeleo ya viwanda na Bandari Kavu ya Kwala, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wawekezaji.
Bw. Twange ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuwezesha ujenzi wa takribani viwanda 200 vya awali katika eneo hilo, ambavyo vinahitaji nishati ya uhakika kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na viwanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Dismas Massawe, amesema kuwa laini hiyo ya kilovolti 33 ina uwezo wa kubeba hadi megawati 50, na hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya Bandari Kavu ya Kwala na Kongani ya Viwanda.
Naye Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani, Mhandisi Cosmas Mkaka, amesema kuwa TANESCO imejipanga kuhudumia viwanda vyote katika Kongani ya Kwala ili kuhakikisha vinapata umeme wa uhakika muda wote, jambo litakalosaidia kuvutia uwekezaji zaidi katika eneo hilo.
Hafla hiyo ilijumuisha uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala, uwekaji wa jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda, pamoja na uzinduzi wa safari ya kwanza ya treni ya mizigo kupitia reli ya kisasa (SGR).