Fadlu aliamsha Simba, Kapombe akiachiwa msala

BAADA ya aliyekuwa nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kutimka kikosini humo inaelezwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids amemwachia msala Shomari Kapombe kwa kupendekeza beki huyo mkongwe kuvaa kitambaa cha unahodha.

Tshabalala ameondoka Simba baada ya miaka 14 na inatajwa amemalizana na Yanga na atakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu 2025/26 na alikuwa nahodha wa timu hiyo msimu uliopita alipompokea John Bocco aliyekuwa amemaliza mkataba na kutua JKT Tanzania.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti, kocha Fadlu amependekeza Kapombe kuwa mbadala wa Tshabalala katika nafasi ya unahodha na hasa baada ya nahodha mwingine msaidizi, Fabrice Ngoma kuondoka kikosini hivi karibuni.

“Mapendekezo ya kocha ni Kapombe, kazi iliyobaki ni wachezaji wenyewe kumpigia kura na kumpitisha kuchukua nafasi hiyo lakini tayari kocha ameonyesha nia ya kumhitaji Kapombe kuwa nahodha wa Simba.”

Wakati Mwanaspoti likinasa taarifa hizo limefanya mahojiano na nyota wa zamani wa timu hiyo ambao wameunga hoja za kocha huyo kumteua Kapombe wakiweka wazi anastahili kutokana na nidhamu, ukongwe na ubora alionao.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel ameshtushwa na taarifa za kuondoka kwa Tshabalala ambaye amekiri kuwa bado alikuwa anahitajika ndani ya Simba huku akiweka wazi kuwa ni muda wa Kapombe kuvaa kitambaa.

“John Bocco alipewa kitambaa kwa heshima tu kwa sababu ni mchezaji ambaye alikuja na kuondoka lakibi Tshabalala alikuwa mtusahihi na sasa ni Kapombe hii ni kutokana na ukongwe wake nidhamu na ubora alionao,” alisema na kuongeza;

“Namtakia kila la kheri Tshabalala alikuwa kiongozi sahihi na bado alikuwa na nafasi ya kuipambania nembo ya Simba, ni wakati wa Kapombe ukiacha nidhamu, bado ana kiwango kizuri  ambacho amedumu nacho kwa muda mrefu ni mtu sahihi kupewa kitambaa.”

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawassa ameungana na Fadlu akiweka wazi, Kapombe anastahili kwa mengi ukongwe, ubora na uzoefu mkubwa alionao sambamba na kudumu kwa kiwango kwa miaka mingi.

‘’Simba ina wachezaji wengi wazawa, lakini kwangu Kapombe anastahili na ndiye mwenye nafasi kubwa japo kocha ndio mwenye uamuzi nani anafaa kufanya naye kazi kulingana na umuhimu wake kikosi cha kwanza,” alisema Pawassa na kuongeza;

“Kapombe ana sifa zote za kuvaa kitambaa ndani ya kikosi cha Simba anastahili amehudumu muda mrefu, ni muda wa kuenziwe ili asukume hilo gurudumu baada ya Tshabalala kuondoka.”

“Lakini suala za unahodha linatazamwa zaidi na kocha kwa sababu yeye ndiye anajua anamtumiaje mchezaji huyo huwezi kuwa na mchezaji kiongozi ambaye anakaa benchi hivyo tunamwachia yeye ndiye atakayeamua.”

Kazi kubwa aliyonayo Kapombe ni kuhakikisha anakwepa mtego wa Tshabalala na tangu aachiwe kitambaa na Bocco, hajatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii wala Kombe la FA.