Yoga ni zoezi maarufu duniani lililobuniwa na wahenga wa nchini India, kiasi cha kulifanya kuwa zoezi la kitamaduni na hatimaye kuwa maarufu nchini humo na nje ya nchi.
Mamilioni ya watu duniani hulifanya sehemu ya maisha yao kwa ajili ya kuboresha afya ya mwili kiujumla ikiwamo afya ya akili. Hii ni kutokana kuhusisha utendaji wa kimwili, kiakili na kiimani.
Ni zoezi kongwe lililofanywa katika karne ya 5 na 6 na wahenga wa Kihindi miaka 3000 BCE iliyopita, ambalo wanasayansi watafiti wamelifanyia na kuonesha kuwa na faida lukuki za kiafya.
Linahusisha mashirikiano ya mazoezi ya kupumua, kuvuta hisia na uamshaji wa hamasa na kuleta utulivu hatimaye kuupa mwili matokeo makubwa kiafya.
Dini za kihindi, buddha na Jaini huamini kuwa ni tiba mbadala wa matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwamo matatizo ya moyo na akili.
Tafiti zinazochapishwa mara kwa mara miaka ya karibuni katika majarida ya kisayansi ikiwamo JAMA, Lancet na mitandao ya kisayansi kama vile Medical News Today na Health line yanaonyesha zoezi hili kusaidia kutibu magonjwa kadhaa ikiwamo ya kimwili na kiakili.
Matokeo ya kitafiti yanaonyesha kuwa zoezi hili linasaidia kupunguza makali na kuondoa shinikizo la akili na kuchochea utulivu wa akili.
Hii ni kutokana na kusaidia kupunguza uzalishwaji kwa kichochezi cha cortisol ambacho kinahusika katika kuchochea shinikizo mwilini.
Utafiti mmoja wa mwaka 2009 unaonyesha kwa wanawake 24 ambao walikuwa na shinikizo la akili walipopewa programu ya miezi mitatu, walionekana katika miili yao kushuka kwa kiwango cha cortisol.
Hatimaye kundi hili la wanawake walionekana kupunguza shinikizo la akili, hofu, uchovu na sonona.
Pia husaidia kuongeza wepesi, kuimarisha misuli, kuboresha upumuaji na nguvu, kusaidia kutunza ubora wa shughuli mbalimbali za mwili, kupunguza uzito, kuboresha mzunguko wa damu na afya ya moyo na kupunguza mwili kujeruhiwa kirahisi.
Vile vile husadia kuondoa maumivu ya mwili, kuchochea ulaji vyakula kwa kuzingatia kanuni za afya.Zoezi hili huwasaidia wagonjwa wa kipanda uso kuepukana na kadhia hiyo.
Faida nyingine ni pamoja na kusaidia kuboresha utulivu wa mwili katika mhimili wake na mwendo kwa watu wazima.
Zoezi hili kama ilivyo mengine hufanywa na rika zote na huwa na faida kubwa kiafya endapo mtu atalifanya angalau kwa dakika 30 kuendelea.
Yoga huwafaa sana wazee; hii ni kutokana na ufanyikaji wake huivuta misuli kwa nguvu ya wastani, hivyo kuwasaidia kuwa wepesi hatimaye kuweza kutembea vizuri pasipo kujikwaa na kujijeruhi.