Dar es Salaam. Tume ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema imezifanyia kazi changamoto mbalimbali mawakala katika chaguzi zilizopita na kuwa hazitatokea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Hakikisho hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima Ramadhani leo Ijumaa, Agosti 1, 2025 jijini Dar es Salaam katika Kikao baina ya tume hiyo na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kailima alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mmoja wa wahariri juu ya tatizo ambalo limekuwa likijitokeza kwenye uchaguzi la mawakala kuzuiwa au kucheleweshwa vituoni na kuruhusiwa uchaguzi ukiwa umekwishaanza.

Katika majibu yake, Kailima amesema: “Angalia mwenendo wa tume wakati wa uchaguzi mdogo, hakukuwa na changamoto za mawakala, tumekwisha kujirekebisha kutokana na changamoto zile.”
Aidha, amesema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, amevitaka vyama kuhakikisha vinawasilisha majina ya mawakala kwa wasimamizi wa uchaguzi siku saba kabla ya siku ya kupiga kura ambayo itakuwa Oktoba 22, 2025 na kuwa wataapisha kwenye kata.
“Tunawaomba ninyi wahariri, mvihamasishe vyama vya siasa kuhakikisha vinawasilisha majina ya mawakala kwa mujibu wa sheria yaani Oktoba 22,” amesema Kailima.

Mbali na hilo, mkurugenzi huyo wa uchaguzi amesema, jumla ya vituo ya kupigia kura 99,911 vitatumika. Kati ya vituo hivyo, 97,349 vipo Tanzania Bara na 2,562 vipo Zanzibar.
Vituo hivyo ni ongezeko la vituo 18,344 kutoka vituo 81,567 vilivyotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Awali, akifungua Kikao hicho, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele amesema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri ikiwemo kukutana na makundi mbalimbali.