Kesi mtoto wa Askofu Sepeku dhidi ya Kanisa la Anglikana kuunguruma leo

Dar es Salaam. Kesi ya Bernardo Sepeku ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku aliyekuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, inaendelea leo Ijumaa, Agosti 1, 2025 Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi.

Bernado alifungua kesi ya madai Mahakama hapo, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Pia, anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Mlalamikaji huyo alifungua kesi hiyo ya madai namba 378/2023, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Angilana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Katika shauri hilo, mtoto huyo aliwasilisha maombi matatu likiwemo la kupinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja namba 2689 chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke ambacho anadai mwaka 1978, waumini na Wakristo wa dayosisi hiyo, walimpa Askofu Sepeku kama zawadi.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa leo Ijumaa Agosti Mosi, 2025 mbele ye Jaji Arafa Msafiri anayesiliza shauri hilo.

Kesi hiyo inaendelea ambapo wajibu maombi wataendelea kutoa ushahidi dhidi ya Sepeku.

Sepeku anatetewa na mawakili kutoka kampuni ya uwakili ya Diakonus Attorneys, Deogratias Butawantemi na Gwamaka Sekela, huku wajibu maombi wao wanatetewa na wakili Dennis Malamba.

Tayari mashahidi wawili wa wajibu maombi wameshatoa utetezi wao mahakamani hapo.

Miongoni mwao ni Katibu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mchungaji George Lawi ambaye alitoa ushahidi wake dhidi ya mleta madai Sepeku..

Katika utetezi wake aliyoutoa Julai 18, 2025, Lawi aliikana Katiba ya kanisa hilo ambayo ni kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo ya mgogoro wa zawadi ya shamba na nyumba alizopewa marehemu  John Sepeku.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa madai uliotolewa na mashahidi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na maaskofu wengine wa kanisa hilo, Askofu Sepeku alipewa zaidi hiyo na Dayosisi ya Dar es Salaam mwaka 1980

Pendekezo la kumzawadia Askofu Sepeku shamba na nyumba lilitolewa awali na Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao chake cha Desemba 8, 1978.

‎‎Sinodi ya Dayosisi hiyo katika kikao chache cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia na kuazimia kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi, shamba la eka 20 lililoko Buza wilayani Temeke, Dar es Salaam, na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mchungaji Lawi ambaye aliieleza Mahakama kuwa pia ni Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo nchini (mdaiwa wa kwanza) katika ushahidi wake, alikana kutambua shamba na nyumba hiyo kutolewa kwa Askofu Sepeku kama zawadi.

Alikana kuitambua zawadi hizo kwa Askofu Sepeku katika ushahidi wake wa msingi akiongozwa na wakili wa wadaiwa, Denis Malamba na ushahidi wa nyongeza akihojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa wadai, Deogratius Butawantemi na Gwamaka Sekela.

Mchungaji  Lawi alidai kuwa kwa mujibu wa muundo wa Kanisa hilo, mmiliki wa mali zote ni Bodi ya Wadhamini na Dayosisi au makanisa moja moja ni waangalizi tu na kwamba hivyo Wadhamini ndio wana mamlaka ya kufanya lolote kuhusiana na mali hizo.

Alidai  kwa kuwa Bodi ya Wadhamini hazikiwahi kukaa na kuamua kumpa Askofu Sepeku zawadi hizo, nyumba na shamba (maana hakuna kumbukumbu zozote zinazoonesha hivyo, basi shamba na nyumba hiyo ni mali ya  wadhamini kwa kuwa Dayosisi si mmiliki wa mali hizo haina mamlaka ya kuzigawa.

Hata hivyo, madai yake ni kinyume na Katiba ya Kanisa hilo ya mwaka 1970 iliyokuwa unatumika wakati Askofu Sepeku anapewa zawadi hizo na Sinodi ya Dayosisi baada ya kuridhika pendekezo la Kamati ya Kudumu ya Dayosisi hiyo.

Endelea kufuatilia Mwananchi