Kwa dau hili la la Kante! Simba imedhamiria…

SIMBA juzi usiku ilimtambulisha kiungo mshambuliaji Alassane Kante kwa mkataba wa miaka miwili, lakini usichokijua ni nyota huyo kutoka Senegal ameikamua klabu hiyo mkwanja wa maana.

Kante ni mmoja ya nyota wapya waliosajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano wa 2025-2026, akiwamo beki wa kati kutoka Sauzi, Rushine de Rueck ambao wameshatambulishwa rasmi na kuungana na msafara wa timu ulioenda kambi ya maandalizi Ismailia, Misri.

Kiungo huo aliyekuwa akiitumikia CA Bizertin ya Tunisia ametua Simba baada ya mabosi wa Msimbazi kuununua mkataba aliokuwa nao kwa dau la Dola 170,000 (zaidi ya Sh435 milioni), huku mwenyewe akikubali dau la mshahara wa Dola 8,000 (zaidi ya Sh20 milioni) kwa mwezi.

Kwa hesabu za kawaida, kwa dau hilo la kununuliwa kwa Sh435 milioni, ukichanganya na mshahara wa Sh20 milioni kwa mkataba huo wa miaka miwili, ina maana dau la nyota huyo ni zaidi ya Sh915 milioni, ikiwa ni mmoja wa wachezaji waliosajiliwa kwa kiwango kikubwa cha fedha.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba, kimelifichulia Mwanaspoti, dili la kiungo huyo aliyetua siku chache baada ya Wekundu hao kudaiwa kumkosa Balla Mousa Konte aliyetua Yanga, limeinjiniwa na Rais wa Heshima na Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji.

Inadaiwa, Mo Dewji ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Simba inaleta majembe ya maana baada ya kuwepo kwa kelele nyingi hatoi fedha, jambo lililomfanya hivi karibuni kuibuka na kuzungumza na Wanasimba na kubainisha ametumia zaidi ya Sh87 bilioni tangu alipoingia kama mwekezaji wakati mchakato wa klabu kuendeshwa kwa hisa ukiendelea.

Chanzon hicho kinasema, MO Dewji aliamua kuingilia kati ili kutimiza mapendekezo ya Kocha Fadlu Davids ambaye alifanya mazungumzo naye akitaka kuletewa mashine za maana ili kutimiza malengo ya kuifanya Simba iwe kali zaidi kuliko ilivyofanya msimu uliopita ilipofika fainali ya CAF.

“Dau la usajili la Kante ni Dola 170,000 (sawa na Sh435 milioni), lakini kwa mwezi jamaa atakuwa anakunja Dola 8,000 (zaidi ya Sh20 milioni) mbali na marupurupu mengine,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Mbali na hilo katika mkataba wake amewekewa kipengele cha endapo akicheza asilimia 70 au zaidi katika mechi zote za Simba basi ataongezewa mkataba mwingine.”

Chanzo hicho kilisema usajili wa Simba unaangalia vijana zaidi kama ilivyo kwa Kante aliyezaliwa  Desemba 20, 2000 katika mji wa Ziguinchor, Senegal ili wakifanya vizuri waweze kuisaidia klabu kwa muda mrefu.

“Hiyo ndiyo sababu ya kuweka kipengele cha kuongezewa mkataba, ili kuepusha makosa kama yaliyofanywa msimu uliyopita, kwani kuna baadhi ya wachezaji vijana ambao waliaminiwa moja kwa moja ila wakashindwa kufikia malengo yetu,” chanzo hicho kilisema.