Mama mwenye kisukari fanya haya kabla na baada ya kujifungua

Dar es Salaam. Mara tu mwanamke mwenye kisukari anapopata ujauzito, ufuatiliaji wa sukari unapaswa kuimarishwa.

Viwango vya sukari hubadilika haraka katika kipindi hiki kutokana na homoni za ujauzito, na hivyo kuna haja ya kurekebisha dozi za insulini au dawa zingine mara kwa mara.

Uhudhuriaji wa  kliniki unapaswa kuwa wa mara kwa mara, ukihusisha mtaalamu wa kisukari, daktari wa wanawake, mtaalamu wa lishe na muuguzi mwelekezi.

Zingatia lishe bora, ulaji wa mlo kamili, usipite muda mrefu bila kula, pamoja na mazoezi mepesi ni muhimu kwa kudhibiti sukari.

 Katika miezi mitatu ya mwisho, daktari huangalia ukuaji wa mtoto kwa ukaribu na kuamua namna bora ya kujifungua, hasa kama kuna hatari ya mtoto kuwa mkubwa kupita kiasi.

Baada ya kujifungua, viwango vya sukari vinaweza kushuka kwa haraka. Kwa wanawake waliokuwa wakitumia insulini, dozi inaweza kupunguzwa au kusitishwa kabisa kwa waliokuwa na kisukari cha ujauzito.

Hata hivyo, ufuatiliaji huendelea ili kuhakikisha hali ya sukari inakuwa katika viwango zinavyohitajika.

Wakati wa kunyonyesha ni muhimu kula milo ya kutosha, kwani kunyonyesha kunaweza kuathiri viwango vya sukari. Hii ni kwa sababu kunyonyesha huchukua nishati ya mwili kwa haraka.

Ni muhimu kwa mama kula vyakula vya kutosha kabla na baada ya kunyonyesha, na awe na vitafunwa vya haraka kuongeza sukari karibu yake kila wakati.

Lishe yenye virutubisho kamili si tu inamsaidia mama kurudisha nguvu na uzito wa kawaida baada ya kujifungua, bali pia ni muhimu kwa kudhibiti kiwango cha sukari.

Mama anapaswa kula mlo kamili unaojumuisha wanga wa kutosha, protini, mafuta yenye afya, mboga na matunda kwa kiasi. Anapaswa pia kunywa maji mengi ili kusaidia uzalishaji wa maziwa.

Baadhi ya wanawake hupunguziwa matumizi ya insulini baada ya kujifungua, lakini wengine huendelea kuhitaji kiwango fulani.

Ni muhimu kufanya marekebisho ya dozi kwa kushirikiana na daktari ili kuepuka hali ya kushuka sana kwa viwango vya sukari. Mama hapaswi kubadilisha dawa au dozi bila ushauri wa mtaalamu wa afya.

Pia, kipindi hiki huleta mabadiliko makubwa ya kihisia hivyo msaada wa kihisia kutoka kwa familia, mume, ndugu wa karibu ni muhimu. Msongo wa mawazo au ‘postpartum depression’ unaweza kuathiri udhibiti wa kisukari.

Kwa wanawake wenye kisukari ni muhimu kuzingatia mambo tajwa kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua, ufuatiliaji wa karibu wakati wa ujauzito, malezi salama baada ya kujifungua.

Ushirikiano kati ya mama, familia na watoa huduma za afya na mahudhurio ya kliniki, ni silaha muhimu katika kuhakikisha maisha bora na afya kwa mama na mtoto.