Mawakili, TLS wataka askari aliyemsukuma Lissu kushughulikiwa

Dar es Salaam. Mawakili wa Tundu Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema wamelaani kitendo cha askari wa Jeshi la Magereza kumsukuma mteja wao mahakamani.

Wameiomba Mahakama na Jeshi la Magereza kuchukua hatua kuzuia vitendo vinavyofanywa na askari hao.

Tukio linalolalamikiwa lilitokea Julai 30, 2025 baada ya kuahirishwa kesi ya uhaini inayomkabili Lissu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti Mosi, 2025, mawakili hao pia wamelalamikia utaratibu wa askari hao kuingia mahakamani wakiwa wamefunika nyuso zao na kumzunguka Lissu. Wametoa wito kwa Mahakama kuzuia matendo hayo.

Wakili Rugemeleza Nshala amesema kitendo cha Mahakama kuruhusu askari wa Jeshi la Magereza kuingia mahakamani wakiwa wameficha nyuso zao na kutesa watu ikiwemo kuwasukuma ni kinyume cha sheria.

“Askari wa Magereza wamekuwa wanakuja mahakamani wamejifunika kininja (wakiwa wamefunika nyuso zao) na kuzunguka kizimba kana kwamba Lissu ana hatia. Tulilalamika mbele ya hakimu mara ya kwanza, walikuwa wanakaa naye hata kizimbani, baadaye wametoka sasa wanakizingira kizimba,” amesema na kuongeza:

“Tunasema hii yote inatuma dalili kwamba mahakama zetu siyo huru. Na sisi kama mawakili hatuwezi kukubali kuwa sehemu ya mahakama ambazo haziko huru.”

Amesema Lissu alisukumwa na kila mtu ameona, lakini hawajasikia tamko lolote la mahakama au hatua za kinidhamu na za kiuwajibikaji kwa mahakama kuelekea kwa Jeshi la Magereza au wakuu wa jeshi hilo kuchukua hatua dhidi ya askari hao.

Dk Nshala anasema askari hao kujifunika nyuso zao kunawaruhusu watende matendo hayo bila kujali wako wapi, jambo ambalo anaeleza ni ukiukwaji uhuru wa mahakama na inaonyesha kuna njama chafu dhidi ya mteja wao kumjeruhi au hata kuhatarisha uhai wake.

Amesema mteja wao kwa hali yake hawezi kukimbia akiwa mahakamani na kuhoji inawezekanaje mtu kama huyo kupeleka askari wa kumzingira.

Amesema mawakili wana jukumu la kupaza sauti ili mambo hayo yasitokee, huku akisisitiza mamlaka za Mahakama na Jeshi la Magereza kuchukua hatua.

Amesema bado wana haki ya kuwashtaki askari hao na hata kama wanafunika nyuso zao, watahangaika kuwatafuta kupata utambulisho wao na kuwashtaki kama watu binafsi.

Dk Nshala amesema wao kama mawakilki na maofisa wa Mahakama watahakikisha  wanautoa mfumo wa haki katika mikono ya watu wasioheshimu haki na uhuru wa mahakama.

Wakili Mpale Mpoki amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria na wote wanapaswa kufuata sheria.

“Vitendo vinavyofanywa na askari Magereza visizidi mamlaka ambayo wamepewa na sheria na Katiba inayokataza kumtesa mtu na kumtweza,” amesema.

Kwa upande wake, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) katika tamko lake kimesema vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola chini ya ulinzi wa Jeshi la Magereza ni ukiukwaji wa Katiba ibara ya 12 (20, 13(6) (b) na misingi ya Haki za Binadamu za Kimataifa.

Katika tamko lililosainiwa na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi chama hicho kimeomba kuonana na Jaji Mkuu kujadili na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu haki, usawa na hadhi ya kila mtu.

“TLS inalitaka Jeshi la Magereza kuwajibika mara moja kwa kuzuia askari wanaoficha utambulisho wao, kuingia mahakamani na kuwachukulia hatua za kinidhamu askari wote waliohusika katika shambulio dhidi ya wakili Lissu Julai 30, 2025,” imesema TLS katika tamko hilo.