TIMU za Tanzania Bara zinaendelea kuvuka maji kuja visiwani Zanzibar kufanya usajili wa wachezaji kuboresha vikosi vyao kwa lengo la kujiandaa na msimu ujao wa 2025-26 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baada ya Yanga na Tabora United, sasa ni zamu ya Mbeya City kutua visiwani hapa kwa ajili ya kusaka saini ya beki wa KVZ, Juma Hassan Shaaban ‘James’.
Klabu hiyo imefunga kambi kisiwani hapa kufanya mazungumzo na uongozi wa KVZ kwa lengo la kuondoka na beki huyo, huku ikielezwa kibunda chao hakipo vizuri, hivyo bado hawajafikia mwafaka.
“Kuna hayo mazungumzo yanayoendelea kati ya Mbeya City na KVZ kwa ajili ya kukamilisha dili hilo, bado wanavutana kwenye dau la usajili,” alisema mtu wa karibu na mchezaji huyo.
Alipoulizwa na Mwanaspoti juu ya uwepo wa dili hili hilo, mchezaji huyo amethibitisha ni kweli uongozi wa Mbeya City unahitaji kumsajili lakini bado wanaendelea na mazungumzo.
“Ni kweli timu ya Mbeya City inahitaji kunisajili lakini wametofautiana katika dau la kuondoka na mimi kwani KVZ inahitaji Sh25 milioni ndipo wanichukue ila kwa upande ya timu hiyo imesema itatoa Sh10 milioni kwa hatua ya awali,” alisema James.
Mwanaspoti ilipohitaji kujua uamuzi wake katika hilo upoje, beki huyo alisema anaangalia upepo utakapovumia ikiwa viongozi watafikia makubaliano ataondoka, kikubwa zaidi anachosubiri ni maamuzi kutoka kwa viongozi wake.