KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kesho Jumamosi kitashuka uwanjani katika mechi ya ufunguzi ya michuano ya Fainali za Kombe la Ubingwa wa Nchi za Afrika (Chan) 2024 dhidi ya Burkina Faso, huku kocha wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ akitamba wapo tayari kwa vita.
Tanzania ambao ni wenyeji wa fainali hizo za naner ikishirikiana sambamba na Kenya na Uganda, imepangwa Kundi B na mechi hiyo ya ufunguzi wa michuano hiyo itafanyika kesho Jumamosi kuanzia saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Kocha Morocco katika mkutano na wanahabari kwa ajili ya mechi hiyo ya ufunguzi itrakayopambwa na wasanii mbalimbali akiwamo mkali wa Bongo Fleva, Rayvanny, amesema Stars ipo tayari kupambana ili kupata ushindi mbele ya Burkina Faso.
“Tumejiandaa kiakili, kiufundi,mbinu na tuna kikosi kizuri cha wachezaji mchanganyiko wa vijana na wazoefu na wapo tayari kwa ajili ya kuipeperusha bendera ya Tanzania,” amesema Morocco na kuongeza;
“Kama ilivyo kauli mbiu ya Watanzania inayosema Kombe la Chan limekuja nyumbani na linabakia nyumbani, kwa upande wetu, benchi la ufundi na wachezaji kauli mbiu yetu ni kushinda kila mechi, ambayo inahamasisha kujituma na kulipambania taifa.
“Watanzania niwatoe wasiwasi kwamba tumejipanga na kila Mtanzania nimwalike aje kuangalia mechi ili kuisapoti timu yetu, kesho Jumamosi tunaanza dakika 90 tungoje zitasimama vipi.”
Morocco ambaye ni kocha wa kwanza mzawa kuipeleka timu hiyo katyika fainali hizo baada ya awali Mbrazili, Marcio Maximo na Mrundi Etienne Ndayiragije kuipeleke Stars katika fainali za mwaka 2009 na 2020, amesema hawaangalii ni kitu gani wamekifanya Burkina Faso katika michuano mbalimbali, isipokuwa wamejipanga kulingana na mechi husika, kikubwa ni kuhakikisha Watanzania wanatoka na kicheko Kwa Mkapa.
“Mechi za kirafiki tulizocheza dhidi ya Uganda, Senegal kule Karatu zimetusaidia kuondoa presha kwa wachezaji, pia tunazungumza nao mara kwa mara, naamini hata watakapoingia uwanjani kwa mechi, watakapocheza dakika tano hadi 10 za kwanza naamini watazoea presha na kuona kila kitu kawaida”.
Kocha wa Burkina Faso, Issa Balbone amesema wamejiandaa vizuri na wapo tayari kwa mchezo dhidi ya Taifa Stars.
“Wanafahamu hawajawahi kuvuka hatua nzuri wamekuwa wakiishia makundi lakini mwaka huu wamejiandaa vizuri kuhakisha wanafanya vizuri na kuvuka hatua za juu zaidi,” amesema Balbone.
Amesema anaifahamu Tanzania na amekuwa akifuatilia mashindano ya Ligi Kuu na leo anaamini atakuwa na mechi mzuri na matarajio ni kupata ushindi wa kwanza na hatimaye kufikia malengo ya kuvuka hatua ya makundi.
Kipa wa Stars, Aishi Manula amesema: “Mechi ya kesho dhidi ya Burkina Faso ina hisia kubwa ni ya ufunguzi tupo nyumbani na wengine wametoka sehemu mbalimbali, kama wachezaji tinaheshimu hilo na tunapambana kuonyesha kile wanachokitarajia ukikona katika mechi hiyo.
” Chan ina fursa kubwa kwa wachezaji vijana kuonyesha viwango vyao ili kuonekana na timu nyingine ili vipaji vyao viweze kufika mbali,kama kaka zao tunawashauri ili kuliona hilo.
“Kila mchezaji anapopata jezi ya Stars ajue tupo katika mapambano ya kuhakikisha tunafanya vitu vikubwa,ili mashabiki wakija uwanjani waondoke na furaha,lakini kwa upande wa mashabiki waje kutupa faraja ili watuheshimishe tujione tupo aridhi ya nyumbani kwa wazazi wetu,” amesema Manula, mmoja ya wachezaji waliokuwapo katika fainali za mwaka 2020 zilizofanyika Cameroon.
Kwa upande wa mchezaji wa Burkina Faso, Patrick Malo amesema wamejiandaa vizuri licha ya kuchelewa kuja Tanzania, lakini wapo tayari kwa mechi hiyo kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
Fainali hizo za Nane zitakazofikia tamati Agosti 30 kwa mechi ya kuamua bingwa itakayopigwa jijini Nairobi, inashiriki jumla ya timu za taifa za nchi 19 zikiwamo wenyeji Tanzania, Kenya na Uganda pamoja na watetezi wa taji, Senegal.