Mradi wa EACLC Wazinduliwa Rasmi, Waahidiwa Kuleta Mageuzi ya Kiuchumi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Agosti Mosi, 2025 na kubainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutazalisha ajira zaidi ya 15,000 za moja kwa moja na nyingine 50,000 zisizo za moja kwa moja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Dkt. Samia amesema kuwa zaidi ya vijana 5,000 tayari wamepata ajira kupitia ujenzi wa mradi huo, huku ajira nyingine 10,000 zikitazamiwa kuzalishwa wakati wa uendeshaji wake.

 “Mradi huu utaifanya Tanzania kuwa chaguo la kwanza kwa wafanyabiashara na wasafirishaji kutoka mataifa jirani, na kuchochea biashara ya kikanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), COMESA, SADC na Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA),” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya biashara na usafirishaji, sambamba na miradi mingine mikubwa kama Bandari Kavu ya Kwala, Kongani za Viwanda, na kuanza rasmi kwa safari za mizigo kwa treni ya umeme ya SGR hapo jana.

Rais Samia amesema EACLC ni mradi wa kimkakati uliolenga kutatua changamoto za muda mrefu za biashara na usafirishaji kwa Tanzania na nchi jirani, na utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji.

“Kituo hiki ni fursa ya kuongeza mapato ya Serikali, kukuza makusanyo ya Halmashauri ya Ubungo, na kuongeza fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa nje ya nchi,” amesisitiza.

Aidha, Rais Samia amewaalika wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa zilizopo katika kituo hicho, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), itakayowezesha huduma zote kupatikana kwa mfumo wa “One-Stop Centre.”

“Nawasihi Watanzania kutumia fursa hizi kukuza biashara na kuongeza thamani ya bidhaa zetu katika soko la kikanda na kimataifa,” amesema Rais Samia.

Katika kuhimiza uendelevu wa mradi huo, Rais Samia ametoa wito kwa wawekezaji kuanzisha matawi ya kituo hicho katika maeneo mengine ya kibiashara nchini ili kuchochea ushindani na ukuaji wa biashara.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo anayemaliza muda wake, amepongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Kimara Mavurunza, Bonyokwa hadi Segerea, iliyokuwa kilio cha wananchi kwa zaidi ya miaka 14 tangu iahidiwe mwaka 2010.

“Rais mwaka 2023 uliamua barabara hii iingie kwenye bajeti, ukatoa Shilingi bilioni 3.6 na kwa mara ya kwanza mkandarasi akaingia kazini,” amesema Prof. Mkumbo.

Ameongeza kuwa idadi ya biashara katika jimbo hilo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 kutoka biashara 4,220 mwaka 2020 hadi 8,997 mwaka 2025, jambo linalothibitisha kuwa mazingira ya biashara yameboreshwa kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, amesema utekelezaji wa mradi huo umetumia zaidi ya Shilingi bilioni 282.7 tangu Mei 2023.

Kituo hicho kina jumla ya vizimba 2,060 ambavyo vimeshajazwa na wafanyabiashara mbalimbali.

“Tunatarajia ajira zaidi ya 15,000 za moja kwa moja na zaidi ya 50,000 zisizo za moja kwa moja. Eneo hili lina ukubwa wa mita za mraba 75,000,” alieleza Teri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kituo hicho kina uhakika wa nishati ya umeme na hakuna sababu ya wafanyabiashara kuwa na wasiwasi.

Ameeleza kuwa serikali tayari imeanza kutekeleza miradi mikubwa ya kuboresha miundombinu ya umeme, ikiwemo ujenzi wa njia ya kilovoti 220, na vituo vya kupozea umeme maeneo ya Ununio na Mabibo, ili kuhakikisha uwekezaji unaoendelea Dar es Salaam unakuwa na nishati ya kutosha.

Kukamilika kwa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki ni hatua kubwa kwa Tanzania katika kukuza uchumi wa kikanda, kuzalisha ajira, na kuvutia mitaji mipya, huku Serikali ikiendelea kujenga misingi imara ya uchumi jumuishi na endelevu.