Mzize hatihati ufunguzi Chan 2024

STRAIKA tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Clement Mzize yupo katika hatihati ya kucheza mechi ya ufunguzi ya fainali za michuano ya Kombe la Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika (Chan) 2024 dhidi ya Burkina Faso.

Fainali hizo za Nane tangu kuasisiwa kwa michuano hiyo inatarajiwa kuanza rasmi kesho Jumamosi kwa pambano la wenyeji Tanzania dhidi ya Burkina Faso kuanzia saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amenukuliwa mapema leo asubuhi katika mkutano wa maandalizi ya mechi hiyio ya ufunguzi, akisema kuwa Mzize yupo katika hatihati ya kucheza pambano hilo kutokana na kuwa majeruhi.

Mzize anayekipiga Yanga hajapata nafasi ya kucheza mechi yoyote kati ya miwili ya kirafiki ya Stars iliyopigwa jijini Arusha katika michuano maalumu kujiandaa na fainali hizo ikishiriki nchi tatu za Tanzania, Senegal na Uganda na Morocco amekiri kuwa ana matatizo kidogo.

“Timu ipo tayari kwa ajili ya kupambania kombe la Chan 2024 na wachezaji kwa asilimia 90 wapo katika hali nzuri isipokuwa Mzize ambaye hatma yake ipo kwenye mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo kesho Jumamosi,” amesema Morocco na kuongeza;

“Vipimo vya mwisho juu yake vitatolewa leo Ijumaa na tutajua kama atakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mechi ya ufunguzi kesho dhidi ya Burkina Faso.”

Morocco amesema timu inafanya mazoezi ya mwisho leo saa 1 usiku kwenye viwanja vya Gymkhana hapo ndio watakapokuwa na majibu sahihi ya mshambuliaji huyo kama atakuwa sehemu ya mchezo au ataendelea na matibabu.

Stars kabla ya mchezo wa kesho tayari wamecheza mechi mbili za kirafiki za michuano iliyoandaliwa na Cecafa yenye jina la 3 Nations  ikipigwa jijini Arusha dhidi ya Uganda na kushinda 1-0 na kuifunga senegal kwa mabao 2-1 na kutwaa taji la michuano hiyo.

Fainali za Chan 2024 zimeandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda na zitachezwa katika miji ya Nairobi, Kampala, Dar es Salaam na Zanzibar ikishiriki timu 19 zilizopangwa katika makundi manne na itafikia tamati Agosti 30. Bingwa mtetezi wa sasa ni Senegal.