Jeshi la Polisi nchini linaeleza limejipanga kwa kiwango cha juu kuhakikisha usalama katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024, huku likionya vikali wale wote watakaotumia mashindano hayo kufanya vitendo vya kihalifu kama wizi, uporaji au uhalifu ndani au nje ya viwanja.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kesho Agosti 2, 2025 hadi 30 na mechi ya ufunguzi ikichezwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Temeke, jijini Dar es Salaam.
Mechi ya ufunguzi itachezwa saa 2 usiku kati ya Taifa Stars dhidi ya Bukinafaso zilizo kundi B pamoja na Mauritania, Madagscar na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Akizungumza na Mwanaspoti, Julai 23, 2025, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro anasema mashindano hayo ni heshima kwa Taifa, hivyo hakuna nafasi kwa watu wanaotaka kuvuruga kwa njia yoyote.
“Tutakuwa na ulinzi wa kutosha maeneo yote ya viwanja, kama kuna mtu anafikiria kuja kufanya fujo ajue mapema tutamshughulikia hapo hapo,” anasema Muliro.
Anasema usalama wa CHAN uko juu ya kawaida, viwanja, hoteli, njia za usafiri, kila eneo limewekwa kwenye tahadhari ya hali ya juu kwa wale wote watakaojaribu kuleta vitendo vya kihalifu kama wizi, uporaji, au fujo watashughulikiwa na hakutakuwa na mjadala.
Muliro pia anasema maandalizi ya barabara zitakazotumika na wageni pamoja na timu zote yameboreshwa kwa kiwango kinachofanana na usimamizi wa mechi kubwa za ndani kama zile za watani wa jadi Simba na Yanga.
“Tuna uzoefu wa mechi za Yanga na Simba, tumeboresha zaidi timu zitakapotoka hotelini hadi uwanjani zitakuwa salama, barabara zitawekwa askari wa kutosha hatutarajii ucheleweshaji, msongamano wala bugudha yoyote,” anasema.
Jeshi limeweka mipango ya ndani na nje ya viwanja vyote vitakavyotumika kwa mashindano hayo, kuhakikisha mashabiki wanapata burudani kwa utulivu bila usumbufu kutoka kwa wahalifu.
Hii inajumuisha kuwepo kwa kamera za ulinzi, askari wa vikosi maalumu na doria za mizunguko.
“Tutakuwepo kila kona, wizi wa simu, pochi, fujo au ulevi wa kupitiliza hautavumiliwa. Mtu akijaribu, tunamkamata hapo hapo hatutasubiri malalamiko,” anaonya.
Muliro anatoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hizo kubwa, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na maelekezo ya vyombo vya usalama.
“Mashindano haya ni heshima kwa Taifa, tujitokeze kwa wingi, lakini kwa nidhamu Polisi tupo kuhakikisha amani inalindwa, lakini kila mtu anayo nafasi ya kusaidia kwa kutofumbia macho uhalifu,” anasema Muliro.
Taswira nzuri ya Tanzania
Anasema kwa mara ya kwanza, Tanzania itakuwa mwenyeji wa CHAN kwa mtindo huu mkubwa, huku mashabiki kutoka mataifa mbalimbali wakitarajiwa kufika kushuhudia kipute hicho.
“Mechi ya ufunguzi itafanyika katika uwanja mkubwa zaidi nchini huku viongozi wa serikali, mashirika ya kimataifa na wageni waalikwa wakitarajiwa kuhudhuria, jambo linaloongeza umuhimu wa usalama na utulivu katika kipindi chote cha mashindano,” anasema.
Upande wa mashabiki wameeleza wasiwasi wao uliokuwepo awali kwani wengi wao wemkuwa na uoga kwa mechi za usiku kwa kuhofia wizi.
Mkazi wa Mbagala Zakhem, Hussein Salum anasema kutokana na ushuhuda wa watu kuibiwa vitu vyao amekuwa na uoga wa kufika uwanjani na huishia kuangalia kwenye runinga.
“Nimekuwa shuhuda ya watu kuibiwa baada ya kumalizika kwa mechi kutokana na kutokuwepo kwa usalama wa kutosha na giza katika maeneo tunayopita pindi tunapohangaika na usafiri,’ anasema Salum.
“Kama Kamanda Muliro ametuhakikishia usalama wetu sawa na isiwe uwanjani ndani tu hadi nje maana wizi asilimia kubwa unafanyika nje ya uwanja eneo la uwanja wa zamani pia waweke taa za kutosha kwa kipindi hiki,” anasema.
Janeth Mbwambo, mkazi wa Gongo la Mboto anasema; “Kitu cha kwanza kinachotufanya tuogope ni misongamano na uhalifu wakati wa kutoka uwanjani.”
Yusuph Kingazi, mkazi wa Buguruni Kisiwani anasema “Kwenye mechi kubwa huwa tuna hofu ya foleni mechi inaisha saa 4 usiku hadi unafika nyumbani saa 6 au 7 usiku kwa sababu ya foleni iliyopo Barabara ya Mandela.”
Anatoa wito kwa jeshi la polisi kwa muda wa kwenda uwanjani na kurudi pia wajitahidi kuvuta foleni, toafuti na hapo watu wanaweza kuacha kwenda uwanjani kwa kuwa hazichezi timu zao pendwa.