Profesa Lekule ateuliwa kuwa makamu mkuu mpya wa Rucu

‎Iringa. Katika juhudi za kuimarisha upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi nchini, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limemteua Profesa Chrispina Lekule kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu). Uteuzi huo umeweka historia, kwani Profesa Lekule anakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika chuo hicho.

‎Uteuzi huo umetokana na kikao cha 85 cha TEC kilichofanyika tarehe 18 hadi 19 Juni 2025, ambapo ilipitishwa rasmi kuwa Prof Lekule aanze rasmi majukumu yake tarehe 1 Septemba 2025.

‎Profesa Lekule ni msomi mwenye sifa za kipekee na tajiriba ya muda mrefu katika sekta ya elimu ya juu, akiwa amehudumu katika nafasi mbalimbali kitaifa na kimataifa.

‎Pia, anajulikana kwa msimamo wake katika kusimamia maadili, kukuza ubora wa kitaaluma, na uongozi unaolenga mabadiliko chanya katika jamii kupitia elimu.

‎Sambamba na uteuzi huo, viongozi wengine waliothibitishwa na TEC ni pamoja na Profesa Alex Ochumbo ambaye ni  Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Fedha na Utawala, Dk Pius Peter Mgeni ni mweka hazina wa Rucu.

‎Uongozi wa RUCU umetoa pongezi kwa walioteuliwa na kueleza matumaini kuwa wataendeleza juhudi za kuimarisha ubora wa elimu katika chuo hicho.

‎Viongozi hao wamehimizwa kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha RUCU inaendelea kutoa elimu bora, inayozingatia maarifa, maadili na mahitaji ya jamii ya sasa.

‎Wakati huo huo, Rucu limefungua rasmi dirisha la maombi ya udahili kwa mwaka wa masomo 2025–2026 kwa ngazi mbalimbali za elimu katika fani zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya taifa.

‎Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha ni taasisi ya elimu ya juu inayojitahidi kuwa jukwaa la kukuza maarifa, maadili, uongozi na huduma kwa jamii kwa mujibu wa misingi ya Kikristo.