Tawi la hilo jipya la benki ya NBC lipo ndani ya jengo hilo la kisasa la biashara ambalo ujenzi wake ulianza kutekelezwa mnamo mwezi Mei mwaka 2023, ukitajwa kugharimu Shilingi bilioni 282.7 hadi kukamilika kwake. Benki ya NBC ni miongoni mwa taasisi za kifedha zilizofadhili ujenzi wa jengo hilo ikiwa ni utekelezaji wa dhamira yake katika kuchochea biashara, usafirishaji, ajira, na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.
Akikagua jengo hilo, Rais Samia aliyekuwa ameambatana na baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipata wasaa wa kutembelea tawi hilo jipya la benki ya NBC ambapo alipokelewa na maofisa waandamizi wa benki hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw Theobald Sabi.
Katika taarifa yake mbele ya Rais, Bw Sabi pamoja na kumpongeza Rais Samia kwa maono yake ya dhati na uongozi thabiti unaoendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kukuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, alisema uanzishwaji wa tawi hilo jipya kwenye kituo hicho ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuunga mkono nia hiyo ya serikali kupitia utoaji wa huduma bora za kifedha zikiwemo huduma za kimataifa.
“Mheshimiwa Rais uwepo wa tawi hili jipya kwenye kituo hiki cha biashara za kimataifa ni sehemu ya jitihada zetu kama benki katika kusogeza huduma za kifedha kwa wafanyabiashara mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kurahisisha na kuchochea kasi ya ufanyikaji wa biashara kwenye kituo hiki.’’
“Tawi hili linatoa huduma zote za kibenki yaani “fully-fledged branch”, ikiwemo huduma za mikopo na ATM za kisasa zinazowezesha kutoa fedha za Kitanzania na fedha za kigeni (Multi-currency), ili kuendana na mahitaji ya biashara za kimataifa. Pia, kwa kuzingatia tabia na mahitaji ya wateja wetu hapa EACLC, tawi hili litafanya kazi kwa muda za ziada —kama ilivyo kwa Tawi letu la Mlimani City, ambalo hutoa huduma hadi saa 1:00 usiku,’’ alisema.
Zaidi Bw Sabi alimuhakikishia Rais Samia kuwa uwepo wa tawi hilo kwenye kituo hicho utasaidia kurahisisha malipo mbalimbali ya serikali kutoka kwa wafanyabiashara hao na hivyo kuzihakikishia mamlaka mbalimbali za serikali uhakika wa kupokea makusanyo yao kwa urahisi zaidi.
“Benki ya NBC ipo tayari kuwa mshirika wa kweli wa Serikali na sekta binafsi katika kukuza biashara, kuwezesha wajasiriamali, na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya taifa letu.’’ Aliongeza.
Uzinduzi wa tawi hilo la Ubungo unaifanya benki hiyo ya NBC kufikisha idadi ya matawi 22 katika jiji la Dar es Salaam pekee, sambamba na mawakala (NBC Wakala) zaidi ya 7,200, hatua ambayo kwa mujibu wa Bw Sabi inaonyesha dhamira ya dhati katika kuchangia juhudi za Serikali kuimarisha ujumuishaji wa huduma za kifedha, na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kushiriki kwenye sekta rasmi ya fedha.
Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa tatu kushoto) akielezea kuhusu huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa kwenye tawi jipya la benki hiyo lililopo kwenye Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam wakati Rais Samia alipotembelea tawi la benki hiyo wakati akiwa anakagua kituo hicho mapema hii leo. Wengine ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo (wa tatu kulia) na maofisa wengine kutoka serikalini na benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (katikati) akizungumza na maofisa waandamizi pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo tawi jipya la Ubungo lililopo kwenye Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa benki ya NBC tawi jipya la Ubungo lililopo kwenye Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam wakiwa tayari kuwahudumia wateja.