Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiitaka Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo kwenda kujifunza ufanyajibiashara kidijitali katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC), amewataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo ili kujipatia kipato.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Agosti 1, 2025 wakati akizindua rasmi kituo cha EACLC ambacho kimegharimu Sh282.7 bilioni hadi sasa huku ujenzi wake ukijumuisha jumla ya sehemu 2,060 za maduka na ofisi. Mradi unatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 15,000 za moja kwa moja na ajira zisizo rasmi 50,000.
Amesema EACLC haijaanzishwa kushindana na Soko la Kariakoo kwani soko hilo tayari limejijengea jina muda mrefu lakini bado linahitaji kujifunza kutokana na uwepo wa kituo hicho.
“Kuwepo kwa kituo hiki si mshindani wa Soko la Kariakoo. Badala ya kuwa mshinani kiwe mkwalimu wa soko la Kariakoo, ikiwezekana Jumuiya ya wafanyabiashara mje kujifunza namna ya kufanya biashara kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kutopoteza mapato ya serikali,” amesema.
Amesema kwenye kituo hicho hawategemei mapato ya Serikali kuvuja kwa sababu wanatumia teknolojia ya kisasa kufanya biashara.
“Hii itakuwa rahisi kwa serikali kuingia na kuona wanavyofanya kazi. Niwaombe sana njooni msome hapa ili Kariakoo iwe na uwezo wa kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa serikali,” amesema.
Hiyo ni kwa sababu kituo hicho wanatumia mifumo ya kisasa ya kidijitali katika usimamizi wa maghala, ufuatiliaji wa mizigo na usafirishaji jambo ambalo litaleta ufanisi katika biashara.

“Tunatarajia mradi huu kukuza biashara ya kikanda na utaweza kuhudumia wafanyabiashara katika nchi wanachama Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Comesa (Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika), SADC (ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na AfCFTA(Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika),” amesema.
Amesema kupitia kituo hicho wafanyabiashara wataweza kufanikisha shughuli zao kwa urahisi zaidi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali huku kikikuza uhusiano baina ya sekta binafsi ya China na Tanzania.
Pia kitatumika kama eneo la kuhamasisha mauzo ya mazao na bidhaa zilizoongezwa thamani kwenda masoko ya China nan je ya nchi huku akisema ndani ya jingo hilo kuna eneo ambalo kazi ya uongezaji thamani hufanyika kabla ya kupelekwa nje ya nchi.
Amesema akiwa humo alikutana na vijana wa Kitanzania wanaotumia rasilimali za Tanzania kama Mkonge na mazao mengine ya kilimo kutengeneza vifaa vya kuuzwa nje.

Rais Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo kuhusu Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo Jijini Dar es Salaam leo Agosti 1, 2025.
“Nimekuta vifaa vizuri vimetengenezwa na ninawashukuru wawekezaji kwa kuwapa nafasi vijana wa kitanzania kuweka vitu walivyo tengeneza kwenda masoko ya nje na niwaombe vijana watumie fursa hiyo,” amesema.
Kufuatia hilo amewataka wazalishaji nchini kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaoendana na hadhi ya jina la Tanzania.
“Zalisheni kwa viwango, nisisitize kuzalisha kwa viwango sababu bidhaa yoyote itakayotoka na alama au maneno kwamba imezaliwa Tanzania lazima itoke na viwango kama jina letu lilivyo na viwango,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi mara baada ya kufungua Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo Jijini Dar es Salaam leo Agosti 1, 2025.
Amesema mradi huo pia utafungamanisha wasambazaji, wazalishaji na walaji ndani nan je ya nchi huku akisema uwepo wa maghala, huduma zote za usafirishaji na ofisi za biashara katika eneo moja kutapunguza gharama na muda wa kusafirisha mizigo.
“Hali hii itafanya bidhaa za Tanzania kuwa na ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa. Hili pia litafanya ushindani wa bandari ya Dar es Salaam kuongezeka kwa kupunguza muda wa ushughulikiaji mizigo kutoka siku saba hadi chini ya siku 3,” amesema Samia.
Suala hilo litasaidia jitihada za Tanzania kuwa chaguo namba moja kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa bidhaa Afrika huku akiwasihi wazalishaji kuzingatia ubora za bidhaa wanazozalisha.
“Zingatieni viwango kwa sababu bidhaa yoyote itakayotoka na alama ya kwamba imetengenezwa Tanzania lazima itoke na viwango kama Tanzania ilivyo na viwango. Niwaombe sana wazalishaji mzalishe kwa viwango vinavyokubalika,” amesema Samia.
Amesema kama Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji wote na moja ya hatua ni uanzishaji wa Tiseza (Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania) ambayo inalenga kuimarisha dhana ya huduma katika eneo moja (one stop center) ili wawekezaji wahudumiwe kwa urahisi.
Mkurugenzi wa EACLC, Dk Lisa Xiangyun Wang amesema kituo hicho kitawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kupanua biashara zao kikanda na kimataifa.
“Tunajivunia kuwa kampuni ya kwanza kusafirisha bidhaa bora na za asili kutoka Tanzania kama vile kahawa na asali kwenye soko la China wakati ambao sisu tunaagiza bidhaa muhimu kama vile mashine na bidhaa za matumizi ya kila siku,” amesema.
Amesema kituo hicho ni kikubwa zaidi cha biashara na usafirishaji nchini Tanzania huku kikiwa kimeunganishwa na huduma za forodha, biashara ya mtandaoni, minyororo ya usambazaji.
“Mradi huu utapunguza gharama za biashara kwa kiwango kikubwa, kutengeneza ajira mpya na kuongeza mapato ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa,” amesema Dk Lisa.
Rais Samia amewahimiza vijana kote nchini kutumia fursa za ajira zinazotolewa badala ya kulaumu kwamba Serikali haiwaoni.
“Tunaposema Serikali tunatengeneza mazingira kwa vijana, haya ndiyo mazingira yenyewe. Sasa ni nyinyi kutumia hizi fursa, kutumia kama mnavyoonyesha hapa, kutengeneza vitu tuwauzie nje.
Msitulaumu Serikali hatuoni; kuona kwenyewe ndiyo hivi. Serikali haiwezi kuja kwa mmoja mmoja ikampa hivi, lakini tumetengeneza mazingira, myatumie,” amesema Samia.
Awali, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri, amesema mbali na kufanikisha uwekezaji wa kituo hiki pia wameendelea kushuhudia idadi kubwa ya miradi inayosajiliwa kwa ajili ya uwekezaji.
“Tangu Julai Mosi Tiseza imekuwa ikiendelea na jukumu la usajili. Jumla ya miradi 503 imeletwa nchini yenye thamani ya Dola za Marekani 5.9 bilioni na katika miradi hii Watanzania 107 na wageni 244 na wabia 101. Wizara imetupa lengo la miradi 1500 ifikapo Desemba mwaka huu,” amesema Teri.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema biashara Ubungo sasa inaongezeka kwa kasi ambapo mwaka 2020 kulikuwa na jumla la biashara 4,220 na sasa kuna biashara 8,997 ikiwa ni ongezeko la asilimia 113.
“Maduka pekee mwaka 2020 yalikuwa 2,825 leo yapo 6,449 bila kuhesabu yanayoongezeka kupitia uwepo wa mradi huu maduka 2,060,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amewatoa shaka wafanyabiashara katika kituo hicho kuwa hawatasumbuliwa na suala la umeme kwani serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali itakayoimarisha upatikanaji wa nishati hiyo.
“Kituo hiki, kinatumia megawati 1.7 kwa sasa lakini wapangaji wote wakiingia kitatumia megawati 4. Kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam, tunatumia megawati 678 haya ni matumizi ya juu kabisa kuliko Mkoa wowote Tanzania,” amesema.