SIMBA inaendelea kushusha vyuma kwa ajili ya msimu ujao na safari hii imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa Ulinzi Starlets, Fasila Adhiambo kwa mkataba wa miaka miwili.
Huu utakuwa usajili wa nne kwa Simba Queens baada ya kukamilisha usajili wa beki wa Yanga Princess, Asha Omary, mshambuliaji kutoka Rwanda, Zawadi Usanase na kipa Mganda, Ruth Aturo.
Kiungo huyo raia wa Kenya aliliambia Mwanaspoti juzi tayari amekamilisha kila kitu na sasa rasmi ni mchezaji halali wa Simba.
“Tayari nimesaini miaka miwili, nimefurahi kukamilisha dili hilo,” alisema Adhiambo ambaye alikuwa nchini mwezi uliopita akiwa na kikosi cha Harambee Starlets kilichocheza fainali ya CECAFA Senior Women’s Championship dhidi ya Tanzania.
Msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Kenya, kiungo huyo alifunga mabao saba na kutoa asisti 17, akitajwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri msimu huo.
Katika eneo la kiungo mshambuliaji, ambapo ndilo eneo asili analocheza Adhiambo, Simba tayari imeachana na Precious Christopher na ujio wake unaweza kuongeza kitu kwenye kikosi cha Msimbazi.
Akiwa na umri wa miaka 20, uwezo wake wa kutengeneza nafasi na kufunga pia unaweza kuwasaidia Simba, ambao kwenye eneo hilo wanahitaji urahisi kwa washambuliaji wao.
Awali Simba ilimfuata, lakini kulikuwa na ugumu hasa kwa upande wa baba yake mzazi ambaye alitaka binti yake aendelee kucheza Ulinzi Starlets ili aweze kupata nafasi ya kuajiriwa jeshini na si kucheza soka la kulipwa.